YouVersion Logo
Search Icon

Wimbo Ulio Bora 8

8
1Laiti ungekuwa kaka yangu,
ambaye amenyonyeshwa na mama yangu!
Hivyo, hata kama ningekutana nawe nje,
ningekubusu na hakuna ambaye angenidharau.
2Ningekuongoza na kukufikisha nyumbani kwa mama mzazi,
mahali ambapo ungenifundisha upendo.
Ningekupa divai nzuri iliyokolezwa,
ningekupa divai yangu ya makomamanga yangu.
3Mkono wako wa kushoto u chini ya kichwa changu,
na mkono wako wa kulia wanikumbatia.
4Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu,
msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi,
hadi hapo wakati wake utakapofika.
Shairi la sita
Wanawake
5Ni nani huyu ajaye kutoka mbugani,
huku anamwegemea mpenzi wake?
Bibi arusi
Chini ya mtofaa, mimi nilikuamsha,
pale ambapo mama yako aliona uchungu,
naam, pale ambapo mama yako alikuzaa.
6Nipige kama mhuri moyoni mwako,
naam, kama mhuri mikononi mwako.
Maana pendo lina nguvu kama kifo,
wivu nao ni mkatili kama kaburi.
Mlipuko wake ni kama mlipuko wa moto,
huwaka kama mwali wa moto.
7Maji mengi hayawezi kamwe kulizima,
mafuriko hayawezi kulizamisha.
Mtu akijaribu kununua pendo,
akalitolea mali yake yote,
atakachopata ni dharau tupu.
Ndugu za Bibi arusi
8Tunaye dada mdogo,
ambaye bado hajaota matiti.
Je, tumfanyie nini dada yetu
siku atakapoposwa?
9Kama angalikuwa ukuta,
tungalimjengea mnara wa fedha;
na kama angalikuwa mlango,
tungalimhifadhi kwa mbao za mierezi.
Bibi arusi
10Mimi nalikuwa ukuta,
na matiti yangu kama minara yake.
Machoni pake nalikuwa
kama mwenye kuleta amani.
Bwana arusi
11Solomoni alikuwa ana shamba la mizabibu,
mahali paitwapo Baal-hamoni.
Alilikodisha kwa walinzi;
kila mmoja wao alilipa vipande elfu vya fedha.
12Shamba langu la mizabibu ni shamba langu mwenyewe,
naam, ni shamba langu binafsi!
Basi, Solomoni, wewe ukae na elfu zako za fedha,
na kila mlinzi wa matunda akae na mia mbili zake.
13Ewe uliye shambani,
rafiki zangu wanasikiliza sauti yako;
hebu nami niisikie tafadhali!
Bibi arusi
14Njoo haraka ewe mpenzi wangu,
kama paa au mwanapaa dume juu ya milima ya manukato.

Currently Selected:

Wimbo Ulio Bora 8: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy