YouVersion Logo
Search Icon

Isaya UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu hiki kina jina la mmoja wa manabii maarufu kabisa wa Waisraeli. Isaya alifanya huduma yake ya kinabii kuanzia mwaka wa 750 hadi 700 K.K. Kitabu hiki kina mahubiri ambayo yanalenga muda mrefu wa karibu miaka 300. Kitabu cha Isaya kina baadhi ya mashairi mazuri kushinda yote katika Biblia; vilevile kina maneno ya kutia moyo yenye kuvutia sana ambayo yanajulikana sana. Waandishi wa kwanzakwanza wa Kikristo na hasa wale walioandika maandishi ya Agano Jipya walipenda sana kumkariri Isaya kuonesha jinsi Mungu alivyotekeleza ahadi yake ya kuwakomboa watu kwa kumtuma mwanawe Yesu Kristo ambaye alileta amani ya kudumu milele (Isa 9:6-7; 11:1-9). Waandishi wa Agano Jipya wanafafanua mateso na kifo cha Bwana Yesu Kristo kuwa kukamilika kwa tenzi zile katika Isaya ambazo zinasema juu ya wadhifa na kazi ya pekee ya “Mtumishi wa Mungu” (Isa 49:1-6; 50:1-11; 52:13–53:12). Kitabu chenyewe chaweza kufikiriwa kuwa na mafungu matatu ya mahubiri:
1. Fungu la kwanza lahusika katika sura 1–39. Sehemu hii kubwa ya kitabu cha Isaya yahusika na hali ya nyakati hizo ambapo utawala wa kusini, yaani Yuda na wakazi wa Yerusalemu, ulikuwa umekabiliwa na msukosuko mkali wa dola yenye nguvu ya dunia hiyo, yaani Ashuru. Watu wengi na wakuu wao walimwacha Mwenyezi-Mungu wakaitumikia na kuiabudu miungu mingine. Watu walitegemea kujiunga na Misri pamoja na tawala nyingine dhidi ya Ashuru. Hali hiyo ilimaanisha kwa Isaya kwamba watu walikuwa wamekosa kumtegemea Mungu. Walisahau kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyewaokoa utumwani Misri, wakakiuka sheria yake. Aliwaonya Waisraeli kwamba, kwa kufanya hivyo, walikuwa wanajitayarishia maangamizi.
2. Fungu la pili lahusu sura 40–55. Yanayosemwa katika sura hizi yanahusu nyakati ambazo watu wengi kutoka Yuda walipelekwa uhamishoni, wakawa huko bila kiongozi wala matumaini ya siku za usoni. Nabii anatangaza kwamba Mungu atawapa uhuru watu hao waliokandamizwa. Watarudishwa katika mji wao na nchi yao, ambamo watashiriki hali mpya ijayo. Jambo muhimu katika mahubiri hayo ni kwamba Mungu ambaye huiongoza historia ya ulimwengu ni tofauti na miungu mingine. Yeye ni Muumba wa ulimwengu na mkuu wa mambo yanayowapata binadamu. Atawarekebisha Waisraeli ili watu wengine wapate fanaka. Hayo yatakamilika kwa huduma ya “Mtumishi wa Bwana.” Katika Agano Jipya jambo hilo la “Mtumishi wa Bwana” limekamilika katika nafsi yake Bwana Yesu Kristo.
3. Fungu la tatu, sura 56–66. Hili linalenga hali na mazingira ya kurudi kutoka uhamishoni. Wakimbizi waliporudi makwao walipata taabu nyingi katika mkikimkiki wa kuanza tena maisha mapya. Kosa la kukaa ugenini (taz pia Isaya 2) lilichukuliwa kwamba limesababishwa na kule kutangatanga kwa Waisraeli. Hawakuishi ipasavyo, hawakupata fursa ya kushika maagizo ya Sabato na hawakuwa na msimamo wowote kidini. Katika sehemu hii watu wanapewa matumaini ya hali njema zaidi siku za usoni. Wanahakikishiwa kwamba Mungu atayatekeleza yale aliyoahidi. Hiyo ndiyo Habari Njema kwao.

Currently Selected:

Isaya UTANGULIZI: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy