YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 1

1
1 #1:1 Taz 2Fal 15:1-7; 15:22--16:20; 18:1--20:21; 2Nya 26:1--32:33 Maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na mji wa Yerusalemu, nyakati za utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.
Mungu awakemea watu wake
2Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Sikilizeni enyi mbingu,
tega sikio ee dunia.
Mimi nimewalea wanangu wakakua,
lakini sasa wameniasi!
3Ngombe humfahamu mwenyewe,
punda hujua kibanda cha bwana wake;
lakini Waisraeli hawajui,
watu wangu, hawaelewi!”
4Ole wako wewe taifa lenye dhambi,
watu waliolemewa na uovu,
wazawa wa wenye kutenda maovu,
watu waishio kwa udanganyifu!
Nyinyi mmemwacha Mwenyezi-Mungu,
mmemdharau Mtakatifu wa Israeli,
mmefarakana naye na kurudi nyuma.
5Kwa nini huachi uasi wako?
Mbona wataka kuadhibiwa bado?
Kichwa chote ni majeraha matupu,
na moyo wote unaugua!
6Toka wayo hadi kichwa hamna penye nafuu,
umejaa majeraha na vidonda vitoavyo damu,
navyo havikuoshwa, kufungwa wala kutiwa mafuta.
7Nchi yenu imeharibiwa kabisa;
miji yenu imeteketezwa kwa moto.
Wageni wananyakua nchi yenu mkiona kwa macho,
imeharibiwa kama uharibifu wa Sodoma.#1:7 Sodoma: Kiebrania: Wageni, Taz Kumb 29:33; Yer 49:18.
8Mji Siyoni umeachwa kama kibanda shambani,
kama kitalu katika shamba la matango,
kama mji uliozingirwa.
9Mwenyezi-Mungu wa majeshi asingalituachia wachache,
tungalikwisha kuwa kama watu wa Sodoma,
tungalikuwa hali ileile ya Gomora.#1:9 Gomora: Taz Mwa 19:24; Roma 9:29.
10Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu
enyi watawala waovu kama wa Sodoma!
Sikilizeni mafunzo ya Mungu wetu
enyi watu waovu kama wa Gomora!
11 #1:11-14 Taz Amo 5:21-22 Mwenyezi-Mungu asema hivi;
“Wingi wa tambiko zenu ni kitu gani kwangu?
Nimezichoka sadaka zenu za kondoo wa kuteketezwa
na mafuta ya wanyama wenu wanono.
Sipendezwi na damu ya fahali,
wala ya wanakondoo, wala ya beberu.
12Mnapokuja mbele yangu kuniabudu
nani aliyewataka mkanyagekanyage nyua zangu?
13Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana;
ubani ni chukizo kwangu.
Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya,
Sabato na mikutano mikubwa ya ibada;
sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi.
14Sikukuu zenu za mwezi mpya na nyinginezo
moyo wangu wazichukia.
Zimekuwa mzigo mzito kwangu,
nami nimechoka kuzivumilia.
15“Mnapoinua mikono yenu kuomba
nitauficha uso wangu nisiwaone.
Hata mkiomba kwa wingi sitawasikia,
maana mikono yenu imejaa damu.
16Jiosheni, jitakaseni;
ondoeni uovu wa matendo yenu mbele yangu.
Acheni kutenda maovu,
17jifunzeni kutenda mema.
Tendeni haki,
ondoeni udhalimu,
walindeni yatima,
teteeni haki za wajane.”
18Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Njoni, basi, tuhojiane.
Ingawa mna madoa mekundu ya dhambi,
mtatakaswa na kuwa weupe kama theluji;
madoa yenu yajapokuwa mekundu kama damu,
mtakuwa weupe kama sufu.
19Mkiwa tayari kunitii,
mtakula mazao mema ya nchi.
20Lakini mkikaidi na kuniasi,
mtaangamizwa kwa upanga.
Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.”
Mji uliojaa dhambi
21Jinsi gani mji uliokuwa mwaminifu
sasa umegeuka kuwa kahaba!
Wakati mmoja haki ilitawala humo,
lakini sasa umejaa wauaji.
22Fedha yenu imekuwa takataka;
divai yenu imechanganyika na maji.
23Viongozi wako ni waasi;
wanashirikiana na wezi.
Kila mmoja anapenda hongo,
na kukimbilia zawadi.
Hawawatetei yatima,
haki za wajane si kitu kwao.
24Kwa hiyo asema Bwana Mwenyezi-Mungu,
Mwenye Nguvu wa Israeli:
“Nitawamwagia maadui zangu hasira yangu,
nitawalipiza kisasi wapinzani wangu.
25Nitanyosha mkono wangu dhidi yenu;
nitayeyusha uchafu wenu kabisa,
na kuondoa takataka yenu yote.
26Nitawapeni waamuzi wenu kama kwanza
na washauri wenu kama pale awali.
Ndipo Yerusalemu utakapoitwa ‘Mji wa Uadilifu’
utaitwa ‘Mji Mwaminifu’”
27Mji Siyoni utakombolewa kwa haki,
uadilifu utawaokoa watakaotubu humo.
28Lakini waasi na wenye dhambi
wote wataangamizwa pamoja;
wanaomwacha Mwenyezi-Mungu watateketezwa.
29Mtaionea aibu hiyo mialoni mliyoipenda sana;
mtafadhaika kwa sababu ya bustani mlizofurahia.
30Mtakuwa kama mwaloni unaonyauka majani;
kama shamba lisilo na maji.
31Wenye nguvu watakuwa kama majani makavu,
matendo yao yatakuwa kama cheche za moto.
Watateketea pamoja na matendo yao,
wala hapatakuwa na mtu wa kuwaokoa.

Currently Selected:

Isaya 1: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy