Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 16:20-28

Walawi 16:20-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Naye akiisha kufanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, na hema ya kukutania, na madhabahu, atamleta yule mbuzi aliye hai. Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari. Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani. Na Haruni ataingia katika hema ya kukutania, naye atavua mavazi yake ya kitani, aliyoyavaa alipoingia katika patakatifu, atayaacha humo; naye ataosha mwili wake kwa maji mahali patakatifu, na kuvaa nguo zake, na kutoka, na kusongeza sadaka ya kuteketezwa yake mwenyewe, na sadaka ya kuteketezwa ya watu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu. Na mafuta ya sadaka ya dhambi atayateketeza juu ya madhabahu. Na mtu yule amwachaye mbuzi wa Azazeli aende zake, ataosha nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia katika marago. Na yule ng’ombe wa sadaka ya dhambi, na yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, ambao damu yao ililetwa ndani ifanye ukumbusho katika patakatifu, watachukuliwa nje ya marago; nao watachoma moto ngozi zao, na nyama yao, na mavi yao. Na yeye awachomaye moto atafua nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia maragoni.

Shirikisha
Soma Walawi 16

Walawi 16:20-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

“Aroni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai. Aroni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, ili kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo. Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote mpaka mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani. “Kisha Aroni ataenda ndani ya Hema la Kukutania na kuvua yale mavazi ya kitani aliyoyavaa kabla ya kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu, naye atayaacha pale. Ataoga kwa maji katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake ya kawaida. Kisha atatoka na kutoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yake na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya watu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, na kwa ajili ya watu. Pia atachoma mafuta ya mnyama wa sadaka ya dhambi juu ya madhabahu. “Yule mtu anayemwachia yule mbuzi wa kubebeshwa dhambi ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji; baadaye anaweza kuingia kambini. Yule fahali na mbuzi waliotolewa kwa ajili ya sadaka za dhambi, ambao damu yao ilikuwa imeletwa Patakatifu pa Patakatifu kwa ajili ya kufanya upatanisho, ni lazima watolewe nje ya kambi. Ngozi zao, nyama, na matumbo pamoja na mavi vitateketezwa kwa moto. Mtu atakayevichoma ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji; baadaye ataweza kuingia kambini.

Shirikisha
Soma Walawi 16

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha