Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 16:20-28

Walawi 16:20-28 NEN

“Aroni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai. Aroni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, ili kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo. Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote mpaka mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani. “Kisha Aroni ataenda ndani ya Hema la Kukutania na kuvua yale mavazi ya kitani aliyoyavaa kabla ya kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu, naye atayaacha pale. Ataoga kwa maji katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake ya kawaida. Kisha atatoka na kutoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yake na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya watu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, na kwa ajili ya watu. Pia atachoma mafuta ya mnyama wa sadaka ya dhambi juu ya madhabahu. “Yule mtu anayemwachia yule mbuzi wa kubebeshwa dhambi ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji; baadaye anaweza kuingia kambini. Yule fahali na mbuzi waliotolewa kwa ajili ya sadaka za dhambi, ambao damu yao ilikuwa imeletwa Patakatifu pa Patakatifu kwa ajili ya kufanya upatanisho, ni lazima watolewe nje ya kambi. Ngozi zao, nyama, na matumbo pamoja na mavi vitateketezwa kwa moto. Mtu atakayevichoma ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji; baadaye ataweza kuingia kambini.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha