YouVersion Logo
Search Icon

Yona 1

1
Yona anajaribu kumkwepa Mungu
1Siku moja, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yona, mwana wa Amitai: 2“Ondoka uende Ninewi, ule mji mkuu, ukaukemee, maana nimeona uovu wake ni mkubwa mno.” 3Basi, Yona akaanza safari, lakini akashika njia ya kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu. Akaenda hadi mjini Yopa ambapo alikuta meli moja iko tayari kwenda Tarshishi. Alilipa nauli, akapanda meli, akasafiri na mabaharia hao kwenda Tarshishi ili kumkwepa Mwenyezi-Mungu.
Yona anaaibishwa na watu wa mataifa mengine
4Lakini Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo mkali baharini, ikatokea dhoruba kali, meli ikawa karibu kabisa kuvunjika. 5Mabaharia wakajawa na hofu, kila mmoja akaanza kumlilia mungu wake; wakatupa baharini shehena ya meli ili kupunguza uzito wake. Wakati huo, Yona alikuwa ameteremkia sehemu ya ndani ya meli, akawa amelala usingizi mzito.
6Nahodha akamwendea, akamwambia, “Wawezaje wewe kulala? Amka umwombe Mungu wako; labda Mungu wako atatuhurumia, tusiangamie.”
7Mabaharia wakasemezana: “Tupige kura tujue balaa hili limetupata kwa kosa la nani.” Basi, wakapiga kura; kura ikamwangukia Yona. 8Hapo wakaanza kumhoji: “Haya, sasa tuambie! Kwa nini balaa hili linatupata? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? U kabila gani?” 9Yona akawajibu, “Mimi ni Mwebrania; namcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, muumba wa bahari na nchi kavu.” 10Kisha Yona akawaeleza kwamba alikuwa anamkwepa Mwenyezi-Mungu. Kusikia hayo, mabaharia hao wakazidi kujawa na hofu, wakamwambia, “Umefanya nini wewe!” 11Wakati huo wote, bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Basi, wakamwuliza Yona, “Tukufanye nini ili bahari itulie?” 12Yona akawajibu, “Nichukueni mkanitupe baharini, nayo bahari itatulia, maana naona wazi kwamba dhoruba hii imewapata kwa sababu yangu mimi.”
13Mabaharia hao wakajaribu bado kupiga makasia wapate kuifikisha meli yao pwani, lakini hawakufanikiwa kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia. 14Basi, wakamlilia Mwenyezi-Mungu wakisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, twakusihi usituangamize kwa kuutoa uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umefanya upendavyo.” 15Basi, wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, na papo hapo bahari ikatulia. 16Mabaharia hao wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu, wakamtolea sadaka na kuweka nadhiri.
17Kisha, Mwenyezi-Mungu akaamuru samaki mkubwa ammeze Yona, naye akawa tumboni mwa samaki huyo kwa muda wa siku tatu, usiku na mchana.

Currently Selected:

Yona 1: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy