YouVersion Logo
Search Icon

Yobu 37

37
1“Kutokana na hayo, moyo wangu unatetemeka,
na kuruka kutoka mahali pake.
2Sikilizeni ngurumo ya sauti ya Mungu,
na mvumo wa sauti kutoka kinywani mwake.
3Huufanya uenee chini ya mbingu yote,
umeme wake huueneza pembe zote za dunia.
4Ndipo sauti yake hunguruma,
sauti ya Mungu hunguruma kwa fahari
na muda huo wote umeme humulikamulika.
5Mungu hupiga radi ya ajabu kwa sauti yake,
hufanya mambo makuu tusiyoweza kuyaelewa.
6Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya nchi!’
Na manyunyu na mvua, ‘Nyesha kwa nguvu.’
7Hufunga shughuli za kila mtu;
ili watu wote watambue kazi yake.#37:7 Kiebrania: Ili wote walio kazi ya mikono yake watambue.
8Wanyama wa porini hurudi mafichoni mwao,
na hubaki katika mapango yao.
9Dhoruba huvuma kutoka chumba chake,
na baridi kali kutoka ghalani mwake.
10Kwa pumzi ya Mungu barafu hutokea,
uso wa maji huganda kwa haraka.
11Mungu hulijaza wingu manyunyu mazito;
mawingu husambaza umeme wake.
12Kwa amri yake vyote huzunguka huku na huko,
kutekeleza kila kitu anachokiamuru,
kufanyika katika ulimwengu wa viumbe.
13Mungu hutekeleza matakwa yake duniani;
iwe ni kwa ajili ya kuwaadhibu watu,
au kwa ajili ya kuonesha upendo wake.
14“Unapaswa kusikiliza Yobu;
nyamaza, usikilize maajabu ya Mungu.
15Je, wajua jinsi Mungu anavyovipa amri yake,
na kufanya umeme wa mawingu yake ungae?
16Je, wajua jinsi mawingu yanavyoelea angani?
Ndizo kazi za ajabu za yule aliye mkamilifu wa maarifa!
17Wewe wajiona umevaa nguo za joto sana,
wakati upepo wa kusi unaivamia nchi.
18Je, waweza, kuzitandaza mbingu kama yeye
zikawa ngumu kama kioo cha shaba?
19Tufundishe tutakachomwambia Mungu;
maana hoja zetu si wazi, tumo gizani.
20Je, nani anathubutu kumwambia: Nataka kuongea?
Nani aseme apate balaa?
21“Ghafla mtu hawezi tena kuona waziwazi:
Jua limefichika nyuma ya mawingu,
na upepo umefagia anga!
22Mngao mzuri hutokea kaskazini;
Mungu amezungukwa na utukufu wa kutisha.
23Mungu Mwenye Nguvu asiyeweza kufikiwa na mtu,
uwezo na uadilifu wake ni mkuu,
amejaa wema wala hapotoshi haki kamwe.
24Kwa hiyo, watu wote humwogopa;
yeye hamjali mtu yeyote mwenye kiburi.”

Currently Selected:

Yobu 37: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy