Walawi 16:15-19
Walawi 16:15-19 Biblia Habari Njema (BHN)
“Halafu atamchinja yule beberu wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya watu wote. Damu ya mbuzi huyo ataileta ndani mahali patakatifu sana na kufanya kama alivyofanya na damu ya yule fahali; atainyunyiza juu ya kiti cha rehema, upande wake wa mbele. Hivyo atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya unajisi, makosa na dhambi zote za Waisraeli. Ndivyo atakavyofanya pia kwa ajili ya hema la mkutano lililo miongoni mwa watu hao walio najisi. Wakati Aroni anafanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na jamii nzima ya Israeli, kamwe asiwepo mtu yeyote ndani ya hema la mkutano hadi atakapokuwa amemaliza na kutoka nje. Kisha atatoka na kwenda kwenye madhabahu iliyo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuifanyia ibada ya upatanisho. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na ya yule mbuzi na kuzipaka pembe za madhabahu pande zote. Atainyunyizia madhabahu hiyo damu kwa kidole chake mara saba na hivyo kuiweka wakfu na kuitakasa unajisi wote wa watu wa Israeli.
Walawi 16:15-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya kama alivyofanya kwa damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao. Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli. Kisha atatoka na kwenda katika madhabahu iliyo mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote. Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.
Walawi 16:15-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa damu ya ng’ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao. Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli. Kisha atatoka na kuiendea madhabahu iliyo mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng’ombe, na ya damu ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote. Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.
Walawi 16:15-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kisha atamchinja mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, na kuichukua damu yake nyuma ya pazia, na aifanyie kama alivyofanya kwa damu ya fahali: Atanyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele yake. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu kwa sababu ya unajisi na uasi wa Waisraeli, kwa dhambi zao zozote. Atafanya hivyo kwa ajili ya Hema la Kukutania, ambalo liko miongoni mwao katikati ya unajisi wao. Mtu yeyote haruhusiwi kuwa ndani ya Hema la Kukutania, kuanzia wakati Aroni anapoingia kufanya upatanisho katika Patakatifu pa Patakatifu, hadi atakapotoka nje, baada ya kujifanyia upatanisho yeye mwenyewe na nyumba yake, pamoja na jumuiya yote ya Israeli. “Kisha atatoka aje kwenye madhabahu yaliyo mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atachukua sehemu ya damu ya fahali na sehemu ya damu ya mbuzi, na kuiweka kwenye pembe za madhabahu. Atanyunyiza baadhi ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.