Yohane 4:46-50
Yohane 4:46-50 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu. Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi. Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!” Huyo ofisa akamwambia, “Bwana, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamwambia, “Nenda tu, mwanao ataishi.” Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.
Yohane 4:46-50 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na ofisa mmoja ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Yudea mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa karibu kufa. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule ofisa akamwambia, Bwana, ushuke mtoto wangu asije akafa. Yesu akamwambia, Nenda; mwanao yu hai. Mtu yule akaliamini lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia.
Yohane 4:46-50 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu. Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia.
Yohane 4:46-50 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hivyo Yesu akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwepo na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa. Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.” Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaondoka akaenda zake.