Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 4

4
Yesu na mwanamke Msamaria
1 # Yn 3:22,26 Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, 2#1 Kor 1:17 (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake) 3aliondoka Yudea, akaenda zake tena mpaka Galilaya. 4#Lk 9:52 Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. 5#Mwa 33:19; 48:22; Yos 24:32 Basi akafika katika mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. 6Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. 7Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. 8Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. 9#Lk 9:53 Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawatangamani na Wasamaria.) 10#Yn 7:38,39 Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. 11Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? 12#Yn 8:53 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake? 13#Yn 6:58 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; 14#Yn 6:27,35; Yn 7:37-39 lakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele. 15Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka. 16Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. 17Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; 18kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. 19#1 Kor 14:24,25; Yn 9:17 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! 20#Kum 12:5; Zab 122:1-9 Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. 21#Mk 14:58 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. 22#2 Fal 17:29-41; Isa 2:3 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. 23Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24#Rum 12:1; 2 Kor 3:17 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. 25#Yn 1:41 Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. 26#Yn 9:37; 10:25 Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.
27Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye? 28Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, 29Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Inawezekana kuwa huyu ndiye Kristo? 30Basi wakatoka mjini, wakamwendea. 31Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. 32#Yn 4:34 Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. 33Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? 34#Yn 17:4 Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenituma, nikaimalize kazi yake. 35#Mt 9:37; Lk 10:2 Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yanakuja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. 36Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. 37#Mik 6:15 Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. 38Mimi niliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.
39Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. 40Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. 41Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. 42#1 Yoh 4:14 Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena tunajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.
Yesu arudi Galilaya
43 # Mt 4:12 Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya. 44#Mt 13:57; Mk 6:4; Lk 4:24 Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. 45#Yn 2:23 Basi alipotoka Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu.
Yesu amponya mwana wa ofisa
46 # Yn 2:1-11 Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na ofisa mmoja ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. 47#Lk 7:2 Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Yudea mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa karibu kufa. 48#Yn 2:18; 1 Kor 1:22 Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? 49Yule ofisa akamwambia, Bwana, ushuke mtoto wangu asije akafa. 50Yesu akamwambia, Nenda; mwanao yu hai. Mtu yule akaliamini lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. 51#Mt 8:6 Na alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. 52Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa na nafuu; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha. 53#Lk 19:9; Mdo 16:15,31 Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake. 54#Yn 2:11,23 Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Yudea kwenda Galilaya.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 4: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha