Kutoka 35:10-19
Kutoka 35:10-19 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kila mtu mwenye ujuzi wa kazi fulani miongoni mwenu atakuja kufanya vitu vyote alivyoamuru Mwenyezi-Mungu: Kutengeneza hema takatifu, kifuniko chake na pazia lake, kulabu zake, pau zake, vikalio vyake; sanduku la agano pamoja na mipiko yake, kiti cha rehema, pazia la mahali patakatifu sana; meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; vinara vya taa pamoja na vyombo vyake vyote, taa zake na mafuta yake; madhabahu ya ubani na mipiko yake, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri, pazia la mlango wa hema takatifu; madhabahu ya sadaka za kuteketezwa pamoja na wavu wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, birika na tako lake; vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake, pazia la mlango wa ua; vigingi vya hema takatifu na vya ua pamoja na kamba zake; mavazi yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na ya wanawe, kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani.”
Kutoka 35:10-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo BWANA ameyaagiza; yaani, hiyo maskani na hema yake, kifuniko chake, vifungo vyake, mbao zake, mataruma yake, viguzo vyake na vitako vyake; hilo sanduku, miti yake, hicho kiti cha rehema na lile pazia la sitara; na hiyo meza, miti yake, vyombo vyake vyote na hiyo mikate ya wonyesho; na hicho kinara cha taa kwa mwanga, vyombo vyake, taa zake na hayo mafuta kwa nuru; na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, miti yake, hayo mafuta ya kupaka, huo uvumba mzuri na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani; na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, miti yake, vyombo vyake vyote hilo birika na kitako chake; na hizo kuta za nguo za ua, viguzo vyake, vitako vyake na pazia la lango la ua; na vile vigingi vya maskani, vigingi vya ua na kamba zake na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
Kutoka 35:10-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo BWANA ameyaagiza; yaani, hiyo maskani na hema yake, na kifuniko chake, na vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na viguzo vyake, na matako yake; hilo sanduku, na miti yake, na hicho kiti cha rehema, na lile pazia la sitara; na hiyo meza, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hiyo mikate ya wonyesho; na hicho kinara cha taa kwa mwanga, na vyombo vyake, na taa zake, na hayo mafuta kwa nuru; na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, na miti yake, na hayo mafuta ya kupaka, na huo uvumba mzuri, na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani; na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hilo birika na tako lake; na hizo kuta za nguo za ua, na viguzo vyake, na matako yake, na pazia la lango la ua; na vile vigingi vya maskani, na vigingi vya ua, na kamba zake na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
Kutoka 35:10-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Wote wenye ujuzi miongoni mwenu inawapasa kuja na kutengeneza kila kitu BWANA alichoamuru: Maskani pamoja na hema lake na kifuniko chake, vibanio, mihimili, mataruma, nguzo na vitako; Sanduku la Agano pamoja na mipiko yake, kifuniko cha kiti cha rehema na pazia linalokizuia; meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate ya Wonyesho; kinara cha taa kwa ajili ya mwanga pamoja na vifaa vyake vyote, taa na mafuta kwa ajili ya mwanga; madhabahu ya kufukiza uvumba pamoja na mipiko yake, mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri; pazia la mlangoni mahali pa kuingilia ndani ya maskani; madhabahu ya sadaka za kuteketeza pamoja na wavu wake wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote; sinia la shaba pamoja na tako lake; pazia la eneo la ua pamoja na nguzo zake na vitako vyake, pazia la ingilio la kwenye ua; vigingi vya hema kwa ajili ya maskani pamoja na ua na kamba zake; mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu kwa ajili ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.”