1 Samueli 17:20-25
1 Samueli 17:20-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Kesho yake, Daudi aliamka asubuhi na mapema, na kondoo akamwachia mchungaji. Alichukua chakula na kwenda kama alivyoagizwa na baba yake Yese. Alipofika kwenye kambi ya Waisraeli, aliwakuta wanajipanga kwenye sehemu yao ya vita na wanapiga kelele za vita. Majeshi ya Waisraeli na ya Wafilisti walijipanga tayari kupigana vita, majeshi yakiwa yanakabiliana ana kwa ana. Daudi alimkabidhi chakula mtu aliyetunza mizigo, akawakimbilia wanajeshi, akaenda kwa kaka zake na kuwasalimia. Alipokuwa anaongea nao, Goliathi yule shujaa wa Wafilisti kutoka Gathi alijitokeza mbele ya wanajeshi wa Israeli kama alivyozoea. Naye Daudi alimsikiliza vizuri sana. Waisraeli walipomwona Goliathi, walimkimbia, na kumwogopa sana. Waliambiana, “Je, mmemwona yule mtu aliyejitokeza? Ama kweli, amejitokeza kuwakejeli Waisraeli. Mfalme Shauli atampa mtu yeyote atakayemuua mtu huyo utajiri mwingi. Zaidi ya yote, atamwoza binti yake. Tena, watu wa jamaa ya baba yake watakuwa huru, hawatalipa kodi.”
1 Samueli 17:20-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita. Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili. Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake. Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia. Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana. Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atampa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuufanya ukoo wa baba yake kuwa huru katika Israeli.
1 Samueli 17:20-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita. Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili. Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake. Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia. Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana. Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli.
1 Samueli 17:20-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Asubuhi na mapema Daudi akaondoka, akaliacha kundi la kondoo pamoja na mchungaji, akapakia vitu vile na kuondoka, kama vile Yese alivyokuwa amemwagiza. Akafika kambini wakati jeshi lilikuwa likitoka kwenda kwenye sehemu yake ya kupigania, huku wakipiga kelele za vita. Israeli na Wafilisti walikuwa wakipanga safu zao wakitazamana. Daudi akaacha vile vitu vyake kwa mtunza vifaa, akakimbilia katika safu za vita na kuwasalimu ndugu zake. Alipokuwa akisema nao, Goliathi, yule Mfilisti shujaa kutoka Gathi, akajitokeza mbele ya safu zake na kupiga ile kelele yake ya kawaida ya matukano, naye Daudi akayasikia. Waisraeli walipomwona yule mtu, wote wakamkimbia kwa woga mkuu. Basi Waisraeli walikuwa wakisema, “Je, mnaona jinsi mtu huyu anavyoendelea kujitokeza. Hujitokeza ili kutukana Israeli. Mfalme atatoa utajiri mwingi kwa yule mtu atakayemuua. Pia atamwoza binti yake na atasamehe jamaa ya baba yake kulipa kodi katika Israeli.”