Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 17

17
Daudi na Goliathi
1 # Yos 15:35; 2 Nya 28:18 Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. 2Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. 3Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, huku bonde likiwa katikati. 4#2 Sam 21:19; 1 Nya 20:5; Yos 11:22; 2 Sam 21:22; 1 Nya 8:13; 18:1; 20:8; 2 Nya 26:6; Amo 6:2 Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. 5Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. 6Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega yake. 7#2 Sam 21:19; 1 Nya 11:23 Na mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. 8#1 Sam 8:17; 1 Nya 21:3 Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. 9#1 Sam 11:1 Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. 10#Hes 23:7,8; 2 Sam 21:21; Neh 2:19 Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. 11Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.
12 # Rut 4:22; 1 Sam 16:1,18; Mwa 35:19; 1 Sam 16:10,11; 1 Nya 2:13 Basi Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrata, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina lake Yese; naye huyo alikuwa na wana wanane; na yeye mwenyewe alikuwa mzee siku za Sauli, na mkongwe miongoni mwa watu. 13#1 Sam 16:6; 1 Nya 2:13 Nao wale wana watatu wa Yese waliokuwa wakubwa walikuwa wamefuatana na Sauli kwenda vitani, na majina ya hao wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya, mzaliwa wa kwanza Eliabu, na wa pili wake Abinadabu, na wa tatu Shama. 14Naye huyo Daudi alikuwa mdogo wa wote; na hao watatu waliokuwa wakubwa wakafuatana na Sauli.
15Basi Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu. 16Kwa siku arubaini yule Mfilisti alijitokeza na kusimama mbele asubuhi na jioni.
17Ndipo Yese akamwambia Daudi mwanawe, Haya! Sasa wapelekee ndugu zako efa ya bisi, na mikate hii kumi, ipeleke upesi kambini kwa ndugu zako; 18#Mwa 37:14 mpelekee kamanda wa kikosi chao jibini hizi kumi, ukawaangalie, wako hali gani, kisha uniletee jawabu yao. 19Basi Sauli, na watu wote wa Israeli, walikuwa katika bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.
20Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita. 21Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili. 22Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake. 23#Mwa 43:27; Amu 18:15 Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia. 24Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana. 25#Yos 15:16 Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atampa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuufanya ukoo wa baba yake kuwa huru katika Israeli. 26#1 Sam 11:2; 14:6; Kum 5:26; Yer 10:10 Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? 27Nao watu wakamjibu vivyo hivyo, wakisema, Ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule atakayemwua.
28 # Mwa 37:4; Mit 18:19; 27:4; Mhu 4:4; Mt 10:36; 27:18; Mk 3:21 Naye Eliabu, mkubwa wake, alisikia hapo alipoongea na watu; na hasira yake Eliabu ikawaka juu ya Daudi, akasema, Mbona wewe umeshuka hapa? Na kondoo wale wachache umemwachia nani kule nyikani? Mimi nakujua kiburi chako, na ubaya wa moyo wako; maana umeshuka ili upate kuvitazama vita. 29#Mit 15:1 Naye Daudi akamjibu, Je! Mimi nimekosa nini sasa? Je! Si neno kubwa hilo? 30Naye akamgeukia ili kumwelekea mtu mwingine, akasema naye jinsi ile ile; na watu wakamjibu tena jinsi ile ile kama ya kwanza.
31Na maneno hayo aliyosema Daudi yaliposikiwa, watu wakamweleza Sauli; naye akatuma mtu kwenda kumwita. 32#Hes 13:30; 14:9; Kum 20:1,3; Isa 30:3; Ebr 12:12; 1 Sam 16:18 Daudi akamwambia Sauli, Asifadhaike moyo mtu yeyote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu. 33#Hes 13:31; Kum 9:2 Sauli akamwambia Daudi, Huwezi kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe ni kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake. 34Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, 35mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. 36Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai. 37#1 Sam 7:12; Zab 18:16,17; 138:3; 2 Kor 1:10; 2 Tim 4:17,18; 1 Sam 20:13; 1 Nya 22:11,16 Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Nenda, na BWANA atakuwa pamoja nawe.
38Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii. 39Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua. 40Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti. 41Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. 42#Zab 123:4; 1 Kor 1:27,28; 1 Sam 16:12 Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. 43#1 Sam 24:14; 2 Sam 3:8 Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. 44#1 Fal 20:10,11; Yer 9:23; Eze 28:2-10; 39:17-20 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. 45#2 Sam 22:33,35; 2 Nya 32:8; Zab 124:8; 125:1; Mit 18:10; 2 Kor 10:4; Flp 4:13; Ebr 11:33,34 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. 46#Kum 28:26; Yos 4:24; 1 Fal 8:43; 18:36; 2 Fal 19:19; Isa 52:10 Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47#Zab 44:6,7; Hos 1:7; Zek 4:6; 2 Nya 20:15 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. 48Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. 49Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. 50#2 Sam 21:19; 23:21; 1 Sam 21:9; Amu 3:31; 15:15 Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. 51#Ebr 11:34 Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia. 52#Yos 15:36 Nao watu wa Israeli na wa Yuda wakainuka, na kupiga kelele, nao wakawafuata Wafilisti mpaka Gathi, na mpaka malango ya Ekroni. Nao majeruhi wa Wafilisti wakaanguka kando ya njia iendayo Shaarimu, mpaka Gathi, na mpaka Ekroni. 53Kisha wana wa Israeli wakarudi kutoka katika kuwafukuza Wafilisti, wakateka nyara kambi yao. 54Naye Daudi akakitwaa kichwa chake yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu; lakini silaha zake akaziweka hemani mwake.
55 # 1 Sam 16:21,22 Sauli alipomwona Daudi akitoka ili kumwendea yule Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, Je! Abneri, kijana huyu ni mwana wa nani? Abneri akamjibu, Ee mfalme, kama iishivyo roho yako, mimi sijui. 56Basi mfalme akasema, Uliza wewe, kijana huyu ni mwana wa nani. 57Hata na Daudi alipokuwa akirudi kutoka katika kumwua yule Mfilisti, Abneri alimtwaa, akamleta mbele ya Sauli, akiwa na kichwa chake yule Mfilisti mkononi mwake. 58#Rut 4:22; 1 Nya 2:13-15; Isa 11:1,10; Mt 1:6; Mdo 13:22; Rum 15:12 Basi Sauli akamwuliza, Wewe, kijana, u mwana wa nani? Naye Daudi akamjibu, Mimi ni mwana wa mtumishi wako, Yese, mtu wa Bethlehemu.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 17: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha