Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 2

2
Tuzo za hekima
1Mwanangu, ukiyakubali maneno yangu,
na kuyathamini maagizo yangu;
2ukitega sikio lako kusikiliza hekima,
na kuuelekeza moyo wako upate ufahamu;
3naam, ukiomba upewe busara,
ukisihi upewe ufahamu;
4ukiitafuta hekima kama fedha,
na kuitaka kama hazina iliyofichika;
5hapo utaelewa ni nini kumcha Mwenyezi-Mungu,
utafahamu maana ya kumjua Mungu.
6Maana Mwenyezi-Mungu huwapa watu hekima;
kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
7Huwawekea wanyofu akiba ya hekima safi,
yeye ni ngao kwa watu waishio kwa uaminifu.
8Huilinda mienendo ya watu watendao haki,
na kuzihifadhi njia za waaminifu wake.
9Ukinisikiliza utafahamu uadilifu na haki,
utajua jambo lililo sawa na jema.
10Maana hekima itaingia moyoni mwako,
na maarifa yataipendeza nafsi yako.
11Busara itakulinda,
ufahamu utakuhifadhi;
12vitakuepusha na njia ya uovu,
na watu wa maneno mapotovu;
13watu waziachao njia nyofu,
ili kuziendea njia za giza;
14watu wafurahiao kutenda maovu,
na kupendezwa na upotovu wa maovu;
15watu ambao mienendo yao imepotoka,
nazo njia zao haziaminiki.
16Hekima itakuwezesha kumkwepa mwanamke mwasherati,
mwanamke malaya wa maneno matamu;
17mwanamke amwachaye mwenzi wa ujana wake,
na kulisahau agano la Mungu wake.
18Nyumba yake yaelekea kuzimu,
njia zake zinakwenda ahera.
19Yeyote amwendeaye kamwe harudi,
wala hairudii tena njia ya uhai.
20Kwa hiyo utafuata mfano wa watu wema,
na kuzingatia mienendo ya waadilifu.
21Maana wanyofu wataipata nchi,
na waaminifu watadumu ndani yake.
22Lakini waovu wataondolewa nchini,
na wenye hila watangolewa humo.

Iliyochaguliwa sasa

Methali 2: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha