Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yuda 1

1
Salamu
1 # Mt 13:55; Mk 6:3 Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, kwa hao walioitwa, waliopendwa katika Mungu Baba, na kuhifadhiwa kwa ajili ya Yesu Kristo. 2#2 Pet 1:2 Mwongezewe rehema na amani na upendano.
3 # 1 Tim 1:18; 2 Pet 1:5; 2:21 Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, niliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. 4#Gal 2:4; 2 Pet 2:1 Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.
Hukumu kwa waalimu waongo
5 # Kut 12:51; Hes 14:29-30,35; 1 Kor 10:5; 2 Pet 1:12 Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kujua haya yote, ya kwamba Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasioamini. 6#Mwa 6:1; Yn 8:44; 2 Pet 2:4,9 Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu. 7#Mwa 19:1-24; 2 Pet 2:6,19 Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kandokando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele. 8#2 Pet 2:10 Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu. 9#Kum 34:6; Dan 10:13,21; 12:1; Zek 3:2; Ufu 21:7; 2 Pet 2:11 Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee. 10#2 Pet 2:12 Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili. 11#Mwa 4:3-8; Hes 22:1-35; 16:1-35; 31:16; 2 Pet 2:15 Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya malipo, nao wameangamia katika maasi ya Kora. 12#Eze 34:8; 2 Pet 2:13 Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa; 13#Isa 57:20; 2 Pet 2:17 ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.
14 # Mwa 5:18,21-24; Kum 33:2; Zek 14:5 Na Henoko, mtu wa kizazi cha saba toka kwa Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana yuaja na watakatifu wake, maelfu kwa maelfu, 15#Mt 25:31 ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno yote maovu ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake. 16#2 Pet 2:10,18 Watu hawa ni wenye kunung'unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.
Maonyo na mahimizo
17 # 2 Pet 3:2 Bali ninyi, wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, 18#2 Pet 3:3,5; 1 Tim 4:1 ya kwamba waliwaambia ya kuwa, Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa za upotevu wao wenyewe. 19#1 Kor 2:14 Watu hao ndio waletao utengano, watu wa dunia hii tu, wasio na Roho. 20#Kol 2:7; 1 The 5:11 Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, 21jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele. 22Wahurumieni wengine walio na mashaka, 23#Amo 4:11; Zek 3:2; Yak 5:19; Ufu 3:4 na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.
Baraka
24 # 1 The 5:23; Flp 1:10; 2 Pet 3:14 Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu; 25#Rum 16:27; 1 Tim 1:17; 2 Pet 3:18 Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina.

Iliyochaguliwa sasa

Yuda 1: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha