Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya UTANGULIZI

UTANGULIZI
Jina Isaya maana yake ni “wokovu hutoka kwa BWANA”. Nabii Isaya ni mwana wa Amozi mzawa ya Yerusalemu. Alikuwa ameoa na kujaliwa watoto wawili (7:3; 8:3). Isaya pia alikuwa na uhusiano kiukoo na mfalme (37:2; 38:1; 39:3). Isaya ni mmojawapo wa manabii maarufu katika Agano la Kale (8:1). Anashuhudiwa kuwa mwenye imani na kupenda watu wamtegemee BWANA tu. Alipenda unyofu (1:4; 17; 3:9; 14-15; 5:8-23), na uadilifu katika jamii (7:4-7; 30:15; 37:6-7). Alikuwa na darasa la wenye kumtumainia Mungu (8:16-17). Unabii wa kitabu hiki unahusika kwa vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza ni kabla ya uhamisho. Wakati huu ndipo Isaya alipoitwa. Israeli na Yuda zilikuwa na msukosuko kisiasa. Mataifa makubwa yalikuwa karibu kuwavamia. Watu walifanya mbinu na mipango ya kupata misaada ya kivita kutoka kwa mataifa mengine yaliyo makubwa. Isaya alipinga mipango hiyo, alikaza kumwamini na kumtegemea Mungu tu. Kutegemea mataifa ni kujiangamiza wenyewe (1-39).
Kipindi cha pili Wayahudi walikuwa uhamishoni Babeli. Wakati huu walikuwa kwenye masikitiko na kukata tamaa. Nabii aitwaye Isaya wa pili, katikati ya karne ya sita Kabla ya Kristo Kuzaliwa anatuliza mioyo ya wafungwa huko Babeli. Anatangaza kuwa Mungu atawapa uhuru, atawarudisha katika nchi yao wakae katika miji yao ya awali na watakuwa na hali mpya. Anawakumbusha uwezo wa Mungu ulio mkuu sana. Hayo yote yatatukia kupitia kwa huduma ya “Mtumishi wa BWANA” (40—55).
Kipindi cha tatu ni baada ya kutoka uhamishoni. Wayahudi walipotoka Babeli wakakaa katika nchi yao walianza kujiuliza maswali kuhusu matazamio yao. Nabii anawatia moyo na kuwapa matumaini ya hali njema zaidi hapo baadaye. Mungu ni mwaminifu atatimiza ahadi zake (56—66).
Nabii Isaya amezungumzia wokovu kuliko wanabii wengine wote.
Yaliyomo:
1. Hukumu ya Mungu kwa Yuda, Yerusalemu na mataifa adui ya Yuda, Sura 1—23
2. Bwana atabariki wanaomtegemea, Sura 24—27
3. Ujumbe kuhusu Hezekia na Waashuri, Sura 28—35
4. Habari za nyongeza kuhusu Hezekia, Sura 36—39
5. Ujumbe wa faraja wa kutoka Babeli, Sura 40—48
6. Kuhusu wokovu, Sura 49—55
7. Maonyo na faraja na utukufu wa wakati ujao, Sura 56—66

Iliyochaguliwa sasa

Isaya UTANGULIZI: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha