Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Torati 3

3
Kushindwa kwa mfalme Ogu
1Ndipo tukageuka, tukakwea njia ya Bashani; na Ogu, mfalme wa Bashani, akatutokea juu yetu, yeye na watu wake wote, kuja kupigana huko Edrei. 2#Hes 21:24 BWANA akaniambia, Usimwogope; kwa kuwa nimemtia mikononi mwako, yeye na watu wake wote na nchi yake; nawe utamtenda kama ulivyomtenda Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni. 3Basi BWANA, Mungu wetu, akamtia mikononi mwako na Ogu mfalme wa Bashani, na watu wake wote; tukampiga, asibakizwe yeyote. 4#Kum 29:8; 1 Fal 4:13 Tukatwaa miji yake yote wakati huo; hapakuwa na mji tusiotwaa kwao miji sitini, nchi yote ya Argobu, ndio ufalme wa Ogu ulio katika Bashani. 5Miji hiyo yote ilikuwa yenye maboma marefu, na malango, na makomeo, pamoja na vijiji visivyokuwa na maboma, vingi sana. 6#Kum 2:24; Zab 135:10-12; 136:19-21 Tukaiharibu kabisa, kama tulivyomfanya huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, kwa kuharibu kabisa kila mji uliokuwa na wanaume, wanawake na watoto. 7Lakini wanyama wote wa mji, na nyara za miji, tulitwaa kuwa mawindo yetu. 8Tukaitwaa na nchi wakati huo, katika mikono ya hao wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ng'ambo ya Yordani, kutoka bonde la Arnoni mpaka kilima cha Hermoni; 9#Zab 29:6; 89:12; 1 Nya 5:23 (na hiyo Hermoni Wasidoni huiita Sirioni, na Waamori huiita Seniri); 10#Kum 4:49; Yos 12:5; 13:11 miji yote ya nchi tambarare, na Gileadi yote, na Bashani yote, mpaka Saleka na Edrei, nayo ni miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani. 11#Amo 2:9; Mwa 14:5; 2 Sam 12:26; Yer 49:2; Eze 21:20; Amo 1:14 (Kwani aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho#3:11 Au, sanduku lake la jiwe alimozikwa. kingali kiko Raba kwa wana wa Amoni? Urefu wake ulikuwa ni dhiraa tisa, na upana wake dhiraa nane, kwa mfano wa mkono wa mtu). 12#Kum 2:36; Yos 12:2; 13:9-12; 2 Fal 10:33; Hes 32:33-38 Na nchi hiyo tuliitwaa ikawa milki yetu, wakati huo; kutoka Aroeri iliyo kwenye bonde la Arnoni, na nusu ya nchi ya milima ya Gileadi, na miji iliyokuwamo, niliwapa Wareubeni na Wagadi; 13#Hes 32:39-42; Yos 13:29; 1 Nya 5:26 na nchi ya Gileadi iliyobaki, na Bashani yote, maana huo ufalme wa Ogu niliwapa nusu ya kabila la Manase; nchi yote ya Argobu, nayo ndiyo Bashani yote. (Na nchi hii yaitwa nchi ya Warefai. 14#1 Nya 2:22; 2 Sam 3:3; 10:6 Yairi, mwana wa Manase, alitwaa nchi yote ya Argobu, hata mpaka wa Wageshuri na Wamaaka; akaziita nchi hizo Hawoth-yairi, kwa jina lake mwenyewe, hata hivi leo, maana, hizo nchi za Bashani.) 15#Hes 26:29; 32:39; Yos 17:1 Na Makiri nilimpa Gileadi. 16#2 Sam 24:5; Hes 21:24 Na Wareubeni na Wagadi niliwapa tokea Gileadi mpaka bonde la Arnoni, katikati ya bonde, na mpaka wake; mpaka mto wa Yaboki, nao ni mpaka wa wana wa Amoni; 17#Hes 34:11; Mwa 13:10; 14:3; Yos 12:3 na nchi ya Araba nayo, na mto wa Yordani, na mpaka wake, tokea Kinerethi mpaka bahari ya hiyo Araba, nayo ni Bahari ya Chumvi, chini ya materemko ya Pisga, upande wa mashariki.
18 # Yos 1:12-15 Nikawaamuru wakati huo, nikawaambia, BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi nchi hii muimiliki, basi vukeni ng'ambo wenye silaha mbele ya ndugu zenu, wana wa Israeli, nyote mlio mashujaa. 19Lakini wake wenu na watoto wenu, na wanyama wenu wa mji, (nawajua kwamba mna wanyama wengi), na wakae katika miji yenu niliyowapa; 20#Yos 22:4 hata BWANA awapumzishe ndugu zenu kama ninyi, nao pia waimiliki nchi wapewayo na BWANA, Mungu wenu, ng'ambo ya Yordani; ndipo mtakaporudi kila mmoja aende katika milki yake niliyowapa. 21Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda BWANA, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda BWANA kila ufalme huko uvukiako. 22#Kut 14:14; Kum 1:30; 20:4 Msiwache, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye.
Musa aitazama Kanaani kutoka Pisga
23 # Hes 27:12-14; Kum 32:48-52 Nikamnyenyekea BWANA wakati huo, nikamwambia, 24#Kum 11:2; Neh 9:32; Zab 106:2; 145:3,6; Yer 32:18-21; Kut 15:11; 2 Sam 7:22; Zab 71:19; 86:8 Ee BWANA Mungu, umeanza kumwonesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu? 25#Kut 3:8; Kum 4:22 Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng'ambo ya Yordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni. 26Lakini BWANA alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; BWANA akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili. 27Kwea katika kilele cha Pisga ukainue macho yako upande wa magharibi, na kaskazini, na kusini, na mashariki, ukatazame kwa macho yako, kwa maana huuvuki mto huu wa Yordani. 28#Hes 27:18; Kum 1:38; 31:3,7 Lakini mwagize Yoshua, mtie moyo na nguvu, umtie na nguvu; kwani ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, na nchi utakayoiona atawarithisha yeye. 29#Kum 4:46 Basi tukakaa katika bonde lililoelekea Beth-peori.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu la Torati 3: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha