Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 8

8
Maono ya kondoo dume na beberu
1Katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake mfalme Belshaza maono yalinitokea mimi, naam, mimi Danieli, baada ya hayo yaliyonitokea hapo kwanza. 2#Neh 1:1; Est 2:8; Mwa 10:22 Nami niliona katika maono; nilipokuwa natazama na nikajionea mwenyewe nikiwa huko Susa, Mji mkuu wa mkoa wa Elamu; nikaona katika maono, nami nilikuwa karibu na mto Ulai. 3Ndipo nikainua macho yangu nikaona, na tazama, mbele ya mto alisimama kondoo dume, mwenye pembe mbili; na pembe zile mbili zilikuwa ndefu; lakini moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, na ile iliyokuwa ndefu zaidi ilizuka mwisho. 4#Dan 11:3 Nikamwona huyo kondoo dume akisukuma upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini; wala hakuna mnyama yeyote awezaye kusimama mbele yake, wala hakuna mnyama yeyote awezaye kupokonya mkononi mwake; lakini alitenda kama alivyopenda mwenyewe, akajitukuza nafsi yake. 5Nami nilipokuwa nikifikiri, tazama, beberu akatoka upande wa magharibi, juu ya uso wa dunia nzima, bila kuigusa nchi; na beberu yule alikuwa na pembe mashuhuri kati ya macho yake. 6Naye akamwendea huyo kondoo dume mwenye pembe mbili, niliyemwona akisimama karibu na mto, akamshambulia kwa ghadhabu za nguvu zake. 7Nikamwona akimkaribia kondoo dume, akamwonea hasira kali, akampiga kondoo dume, akazivunja pembe zake mbili; na huyo kondoo dume alikuwa hana nguvu kusimama mbele yake; bali akamwangusha chini, akamkanyagakanyaga; wala hapakuwapo awezaye kumwokoa kondoo dume katika mkono wake. 8#Dan 7:6 Na yule beberu akajitukuza sana; na alipokuwa na nguvu, pembe ile kubwa ilivunjika; na badala yake zikazuka pembe nne mashuhuri zilizoelekea pepo nne za mbinguni. 9#Dan 11:25; Zab 48:2 Na katika moja ya pembe hizo ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri. 10#Isa 14:13; Dan 11:28; Ufu 12:4 Nayo ikakua, kiasi cha kulifikia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga. 11#Yer 48:26; Dan 5:23; 2 The 2:4 Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini. 12Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa. 13#1 Pet 1:12 Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akinena, na mtakatifu mwingine akamwuliza huyo aliyenena, Haya maono kuhusu habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa liletalo ukiwa, yataendelea hata lini, kukanyaga patakatifu na jeshi? 14Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.
Malaika Gabrieli afasiri maono
15Ikawa mimi, naam, mimi Danieli, nilipoyaona maono hayo, nilitafuta kuyafahamu, na tazama, alisimama mbele yangu mmoja mfano wa mwanadamu. 16#Dan 9:21; Lk 1:19,26 Nikasikia sauti ya mwanadamu katikati ya mto Ulai, iliyoita na kusema, Gabrieli, mfahamishe mtu huyu maono haya. 17#Ufu 1:17 Basi alipakaribia mahali niliposimama; nami niliogopa alipokaribia, nikaanguka kifudifudi; lakini aliniambia, Fahamu, Ee mwanadamu, kwa maana maono haya ni ya wakati wa mwisho. 18Basi alipokuwa akisema nami, nilishikwa na usingizi mzito na uso wangu uliielekea nchi; lakini alinigusa, akanisimamisha wima. 19Akaniambia, Tazama, nitakujulisha yatakayokuwa wakati wa mwisho wa ghadhabu; maana, ni ya wakati wa mwisho ulioamriwa. 20Yule kondoo dume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi. 21Na yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Ugiriki; na ile pembe kubwa iliyo kati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. 22Tena katika habari ya pembe ile iliyovunjika, ambayo badala yake zilisimama pembe nne, falme nne zitasimama kutoka katika taifa lile, lakini si kwa nguvu kama zake. 23#Kum 28:50 Na wakati wa mwisho wa ufalme wao, wakosaji watakapotimia kilele cha uovu wao, mfalme mwenye uso mkali, afahamuye mafumbo, atasimama. 24#Ufu 13:7 Na nguvu zake zitakuwa nyingi mno, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe; naye ataharibu kiasi cha kustaajabisha watu, na kufanikiwa, na kutenda apendavyo; naye atawaangamiza hao walio hodari na watu watakatifu. 25#Ayu 34:20; Omb 4:6 Na kwa mashauri yake atafanikisha hila mkononi mwake; naye atajitukuza nafsi yake moyoni mwake; naye atawaangamiza wengi katika hali yao ya salama; naye atasimama kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu; lakini atavunjika, bila kazi ya mikono. 26#Eze 12:27; Dan 10:14; Ufu 22:10 Na maono ya hizo nyakati za jioni na asubuhi yaliyosemwa ni kweli; lakini wewe yafunike maono hayo; maana ni ya wakati ujao baada ya siku nyingi. 27#Dan 2:48,49 Na mimi, Danieli, nikazimia, nikaugua siku kadhaa; kisha nikaondoka, nikatenda shughuli za mfalme; nami niliyastajabia yale maono, ila hakuna aliyeyafahamu.

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 8: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha