Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 27

27
Paulo asafiri hadi Rumi
1 # Mdo 25:12 Basi ilipoamriwa tuabiri hadi Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya ofisa mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto. 2#Mdo 19:29; 20:4 Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi. 3#Mdo 24:23; 28:2,16 Siku iliyofuata tukawasili Sidoni; Yulio akamfadhili sana Paulo akampa ruhusa kwenda kwa rafiki zake, apate kutunzwa. 4Kutoka huko tukiwa baharini, tukasafiri chini ya Kipro ili kujikinga upepo, kwa maana upepo ulikuwa unatukabili. 5Tulipopita bahari ya upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira, mji wa Likia. 6Na huko yule ofisa akakuta merikebu ya Aleksandria, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo. 7Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone. 8Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea.
9 # 2 Kor 11:25,26; Law 16:29 Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, 10akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia. 11Lakini yule ofisa akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo. 12Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini mashariki na kusini mashariki.
Dhoruba katika bahari
13Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang'oa nanga, wakasafiri karibu na Krete kandokando ya pwani. 14Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo, 15merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. 16Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida. 17Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi. 18Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, kesho yake wakaanza kuitupa shehena baharini. 19Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. 20Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.
21Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. 22Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. 23Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, 24#Mdo 23:11 akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. 25Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa. 26#Mdo 28:1 Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja.
27Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huku na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu. 28Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano. 29Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche. 30Na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu, wakiishusha mashua baharini kana kwamba wanataka kutupa nanga za omo, 31Paulo akawaambia ofisa na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka. 32Basi askari wakazikata kamba za mashua, wakaiacha ianguke.
33 # Mdo 27:27 Na kulipokuwa kukipambazuka Paulo akawasihi wote wale chakula, akisema, Leo ni siku ya kumi na nne kungoja na kufunga, hamkula kitu chochote. 34#1 Sam 14:45; 2 Sam 14:11; Mt 10:30 Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea. 35#Yn 6:11; 1 Tim 4:4; Lk 22:19 Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula. 36Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe. 37Na sisi tuliokuwa ndani ya merikebu tulikuwa watu mia mbili na sabini na sita. 38Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini.
Kuvunjika kwa meli
39Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana. 40Wakazitupilia mbali zile nanga, na kuziacha baharini, pamoja na kuzilegeza kamba za sukani, wakalitweka tanga dogo ili liushike upepo, wakauendea ule ufuo. 41Lakini wakafikia mahali palipokutana bahari mbili, wakaiegesha merikebu, omo ikakwama ikakaa isitikiswe, bali tezi ilikuwa imefumuliwa kwa nguvu za mawimbi. 42Mpango wa askari ulikuwa kuwaua wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia. 43Bali ofisa, akitaka kumponya Paulo, akawazuia, wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea wajitupe kwanza baharini, wafike katika nchi kavu; 44#Mdo 27:22-25 nao waliosalia, hawa juu ya mbao na hawa juu ya vitu vingine vya merikebu. Na hivyo watu wote wakapata kuifikia nchi kavu salama.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 27: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha