Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 6

6
Sulemani ajenga hekalu
1Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya wana wa Israeli kutoka nchini Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika mwezi wa Zivu,#6:1 Zivu ni mwezi wa pili katika kalenda ya Israeli. ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya BWANA. 2#Eze 41:1 Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea BWANA, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini. 3Na ukumbi mbele ya hekalu la nyumba, urefu wake ulikuwa mikono ishirini, kadiri ya upana wa nyumba; na upana wake mikono kumi mbele ya nyumba. 4#Eze 40:16 Akaifanyia nyumba madirisha ya miangaza yenye kimia. 5Nao ukuta wa nyumba akauzungushia vyumba, kushikamana na kuta za nyumba kotekote, za hekalu na za chumba cha ndani; akafanya vyumba vya mbavuni pande zote. 6Chumba cha chini kilikuwa mikono mitano upana wake, na chumba cha katikati kilikuwa mikono sita upana wake, na chumba cha tatu kilikuwa mikono saba upana wake; kwa kuwa upande wa nje akaupunguza ukuta wa nyumba pande zote, ili boriti zisishikamane kutani mwa nyumba. 7Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliyokwisha kuchongwa machimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma chochote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba. 8Mlango wa vyumba vya chini ulikuwapo upande wa kulia wa nyumba; mtu hupanda ngazi za kuzunguka mpaka vyumba vya katikati, na kutoka vile vya katikati mpaka vile vya tatu. 9Basi ndivyo alivyoijenga nyumba, akaimaliza; akaifunika nyumba kwa boriti na mbao za mwerezi. 10Akavijenga vyumba mbavuni mwa nyumba yote, kwenda juu kwake kila kimoja kilikuwa mikono mitano; vikaitegemea nyumba kwa boriti za mwerezi.
11Neno la BWANA likamjia Sulemani, kusema, 12Katika habari ya nyumba hii unayoijenga, kama ukienda katika sheria zangu, na kuzifanya hukumu zangu, na kuzishika amri zangu zote na kwenda katika hizo; ndipo nitakapolithibitisha neno langu kwako, nililomwambia Daudi baba yako. 13#Kut 25:8; 29:45; Law 26:11; Zab 132:13,14; Eze 37:26-28; 2 Kor 6:16; Ebr 3:6; 13:5; Ufu 21:3; Kum 31:6 Nami nitakaa katikati ya wana wa Israeli, wala sitawaacha watu wangu Israeli.
14Basi Sulemani akaijenga hiyo nyumba akaimaliza. 15Akazijenga kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za mberoshi. 16#Kut 26:33; Law 7:6; 16:2; Hes 18:10; 1 Fal 8:6; 2 Nya 3:8; Eze 45:3; Ebr 9:3 Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu. 17Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arubaini. 18Na ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana.
19 # Kut 40:20; 1 Fal 8:6-10 Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la Agano la BWANA. 20Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi. 21Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu. 22#Kut 30:1 Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu.
Mapambo ya hekalu
23 # Kut 25:20; 37:7-9; 2 Nya 3:10-12; 5:8 Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi. 24Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili. 25Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja. 26Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo hivyo. 27#Kut 25:20; 37:9; 2 Nya 5:8 Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba. 28Akayafunika makerubi kwa dhahabu. 29Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje. 30Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje. 31#Yn 10:7 Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano. 32Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. 33Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne; 34#Eze 41:23 na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana. 35Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro. 36Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi.
37Katika mwaka wa nne nyumba ya BWANA ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu.#6:37 tazama 6:1. 38Na katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli,#6:38 Buli ni mwezi wa nane katika kalenda ya Kiyahudi. ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, kulingana na kanuni zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.

Iliyochaguliwa sasa

1 Wafalme 6: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha