Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufu UTANGULIZI

UTANGULIZI
Hiki ni kitabu cha mwisho katika orodha ya vitabu vya Biblia. Kitabu hiki kinafaa sana kumalizia Maandiko yote matakatifu ya Agano la Kale na Agano Jipya maana katika sura zake za mwisho ukamilifu wa ujumbe wa wokovu unaelezwa.
Neno ufunuo ni tafsiri ya Kigiriki “apokalupsis” na maana yake ni “ufunuo” au “ufichuo”. Bali na kitabu hiki katika Biblia kuna maandiko ya kiufunuo, kama vile Ezekieli (1; na 40–48), Danieli (7–12), Zekaria (1–6), Isaya (24–27), Marko (13). Maandiko haya huitwa hivyo kwa kuwa yanatoa ujumbe wake kwa njia ya maono yaliyofunuliwa na Mungu mwenyewe ili kueleza mapenzi yake na siri za mbinguni.
Kitabu hiki cha Ufunuo kina maono ya kweli yanayorudia kwa namna mbalimbali kanuni za utawala wa Mungu wa haki na huruma juu ya ulimwengu wote na viumbe vyote. Kwa kanuni hizo za Mungu Kanisa limetegemezwa na litaendelea kutegemezwa katika misukosuko ya maadui wa kidunia na wa nguvu za pepo waovu.
Ili kuweza kueleza jambo hilo kuu la kanuni za Mungu kuhusu ulimwengu, mwandishi anatumia picha mbalimbali za ishara zikiwamo takwimu na wanyama wa ajabu, ambazo mwandishi anazieleza na kuzifafanua na hivyo kuwawezesha wasomaji wake kuuelewa ujumbe unaotolewa.
Jambo moja kiini katika kitabu hiki ni kwamba mwandishi anashuhudia kufufuka kwake Yesu Kristo, tukio ambalo ni kiini cha imani ya Kikristo na msingi wa tangazo la Injili (rejea 1 Kor 15:14-17) na pia ni ishara timilifu ya kuweko kwa Ufalme wa Mungu. Maandiko ya kiufunuo yanaeleza hali ya mateso makali yanayowakabili watu wa Mungu. Yanalaumu watu wanaosababisha shida na mateso, na kutabiri hukumu yao. Kwa upande mwingine, maandishi hayo yanawafariji na kuwatia moyo wanaoteswa ili wavumilie wakitumaini hali njema watakayopata. Yaani, Mungu ni wa haki naye ataondoa maovu yote, ataadhibu watenda maovu na kwa wakati wake atawaletea heri wale wanaomcha. Katika kueleza hali hiyo waandishi hutumia majina yasiyokuwa halisi ili kukwepa mateso zaidi.
Mwandishi wa kitabu cha Ufunuo anajitaja kuwa ni Yohana. Tangu karne za kwanza baada ya Kristo imekubalika kuwa ndiye Yohana Mtume (tazama utangulizi kwa Injili ya Yohana). Alikuwa amefungwa kwa ajili ya imani na kushuhudia Injili kisiwani Patmo. Yohana akiwa kisiwani humo alipokea maono, akayaandika na kuyatuma kwa makanisa saba yaliyoko katika mikoa ya Asia Ndogo. Makanisa hayo yalikuwa yanateswa. Yohana anawapa ujumbe wa kuwafariji na kuwatia moyo kwamba mwisho wa udhalimu na mateso umekaribia na utawala wa Kristo unaanza. Anasema kuwa punde si punde machozi yatafutika; huzuni, majonzi na uchungu wa kifo vitakomeshwa milele (21:4).

Iliyochaguliwa sasa

Ufu UTANGULIZI: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha