Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zab 119:1-56

Zab 119:1-56 SUV

Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya BWANA. Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote. Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake. Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana. Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako. Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote. Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako. Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Ee BWANA, umehimidiwa, Unifundishe amri zako. Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako. Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi. Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako. Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako. Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako. Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako. Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati. Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako. Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako. Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako. Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu. Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako. Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako. Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako. Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako. Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu. Nimeambatana na shuhuda zako, Ee BWANA, usiniaibishe. Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu. Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho. Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo. Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako. Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako. Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema. Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako. Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako. Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako. Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako. Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele. Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda. Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako. Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha. Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha. Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako. Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee BWANA, nikajifariji. Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako. Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu. Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee BWANA, nikaitii sheria yako. Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.

Soma Zab 119

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zab 119:1-56

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha