Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 20:19-31

Yn 20:19-31 SUV

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.

Soma Yn 20

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha