Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 14:15-31

Yn 14:15-31 SUV

Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.

Soma Yn 14

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yn 14:15-31

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha