Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kut 12:23-51

Kut 12:23-51 SUV

Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele. Itakuwa hapo mtakapoifikilia hiyo nchi, BWANA atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu. Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N’nini maana yake utumishi huu kwenu? Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia. Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama BWANA alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya. Hata ikawa, usiku wa manane BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu. Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni BWANA kama mlivyosema. Twaeni kondoo zenu na ng’ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu, mkanibariki mimi pia. Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote. Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani. Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi. BWANA akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara. Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu sita mia elfu watu waume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto. Na kundi kubwa la watu waliochangamana mno wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng’ombe, wanyama wengi sana. Nao wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula. Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini. Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya BWANA yalitoka nchi ya Misri. Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za BWANA kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa BWANA, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao. BWANA akawaambia Musa na Haruni, Amri ya pasaka ni hii; mtu mgeni asimle; lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha, ukiisha kumtahiri, ndipo hapo atamla pasaka. Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle pasaka. Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yo yote; wala msivunje mfupa wake uwao wote. Na wafanye jambo hili mkutano wa Israeli wote. Na mgeni atakapoketi pamoja nawe, na kupenda kumfanyia BWANA pasaka, waume wake wote na watahiriwe, ndipo hapo akaribie na kufanya pasaka; naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi; lakini mtu ye yote asiyetahiriwa asimle. Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu, na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli wote; kama BWANA alivyowaagiza Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya. Ilikuwa siku ile ile moja, BWANA akawatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri kwa majeshi yao.

Soma Kut 12

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Kut 12:23-51

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha