Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kum 5:1-21

Kum 5:1-21 SUV

Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda. BWANA, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. BWANA hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai. BWANA alisema nanyi uso kwa uso mlimani, toka kati ya moto; (nami wakati ule nalisimama kati ya BWANA na ninyi, ili kuwaonyesha neno la BWANA; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure Jina la BWANA, Mungu wako; maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure. Ishike siku ya Sabato uitakase, kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato. Waheshimu baba yako na mama yako; kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako. Usiue. Wala usizini. Wala usiibe. Wala usimshuhudie jirani yako uongo. Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala kitu cho chote alicho nacho jirani yako.

Soma Kum 5

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha