Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Sam 15:12-26

1 Sam 15:12-26 SUV

Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali. Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na BWANA, nimeitimiza amri ya BWANA. Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng’ombe ninaousikia? Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng’ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia BWANA usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema. Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye BWANA akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Kisha BWANA akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia. Mbona, basi, hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA? Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya BWANA, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali. Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme. Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao. Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu BWANA. Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la BWANA, BWANA naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.

Soma 1 Sam 15

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha