YouVersion Logo
Search Icon

Ufunuo 16

16
Mabakuli ya ghadhabu ya Mungu
1Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani.”
2Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama na wale walioiabudu sanamu yake.
3Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa.
4 # Taz Zab 78:44 Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu. 5Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema,
“Ewe mtakatifu, uliyeko na uliyekuwako!
Wewe umetenda sawa kuhukumu mambo hayo.
6Maana waliimwaga damu ya watu wa Mungu na manabii,
nawe umewapa damu wainywe;
wamestahili hivyo!”
7Kisha, nikasikia sauti madhabahuni ikisema, “Naam, Bwana Mungu Mwenye Nguvu! Hukumu zako ni za kweli na haki!”
8Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake. 9Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo. Lakini hawakutubu na kumtukuza Mungu.
10Kisha, malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu, 11wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakutubu matendo yao mabaya.
12Kisha, malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ikawekwa kwa ajili ya wafalme kutoka mashariki. 13Kisha, nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama na kinywani mwa yule nabii wa uongo. 14Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita ya ile siku kubwa ya Mungu Mwenye Nguvu.
15“Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko na kuaibika hadharani.”
16Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni.
17Kisha, malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, hekaluni, ikisema, “Imetendeka!” 18Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu. 19Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha kikombe cha divai ya ghadhabu ya hasira yake. 20Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena. 21Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.

Currently Selected:

Ufunuo 16: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy