YouVersion Logo
Search Icon

Methali 12

12
1Apendaye nidhamu hupenda maarifa,
bali asiyependa kuonywa ni mjinga.
2Mtu mwema hufadhiliwa na Mwenyezi-Mungu,
lakini mwenye nia mbaya hulaaniwa na Mungu.
3Mtu hawi imara kwa kutenda maovu,
lakini hakuna kiwezacho kumngoa mtu mwadilifu.
4Mke mwema ni taji ya fahari kwa mumewe;
amwaibishaye mumewe ni kama kidonda mifupani mwake.
5Mawazo ya mwadilifu ni ya haki;
mashauri ya mwovu ni ya udanganyifu.
6Maneno ya waovu lengo lake ni kuua,
lakini maneno ya waadilifu huwaokoa wanaotishwa.
7Waovu huangamizwa na kutoweka kabisa,
lakini jamaa ya waadilifu hudumishwa.
8Mtu husifiwa kadiri ya hekima yake,
lakini mtu wa fikira mbaya hudharauliwa.
9Afadhali mtu wa chini anayejitegemea,
kuliko ajitakiaye makuu na kukosa chakula.
10Mtu mwadilifu huwajali wanyama wake,
lakini huruma ya mwovu ni ukatili.
11Mkulima mwenye bidii ana chakula tele,
lakini afuataye mambo yasiyofaa hana akili.
12Waovu hutamani faida isiyo halali,
lakini mtu mwadilifu husimama imara.#12:12 aya ya 12 makala ya Kiebrania si dhahiri na tafsiri yake si hakika.
13Mtu mwovu hunaswa kwa uongo wake mwenyewe,
lakini mwadilifu hutoka katika taabu.
14Mtu hufanikiwa kutokana na maneno yake
kama apatavyo matokeo ya kazi za mikono yake.
15Mpumbavu huiona njia yake kuwa sawa,
lakini mwenye hekima husikiliza shauri.
16Udhia wa mpumbavu hujulikana mara,
lakini mwerevu huyapuuza matukano.
17Msema kweli hutoa ushahidi wa kweli,
lakini shahidi wa uongo hutamka udanganyifu.
18Maneno ya ovyo hujeruhi kama upanga,
lakini asemayo mwenye hekima huponesha kidonda.
19Ukweli hudumu milele,
lakini uongo ni wa kitambo tu.
20Wanaopanga maovu wamejaa udanganyifu moyoni,
lakini wanaonuia mema hupata furaha.
21Waadilifu hawapatwi na jambo lolote baya,
lakini waovu wamejaa dhiki.
22Midomo isemayo uongo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu,
lakini watu waaminifu ni furaha yake.
23Mwenye busara huficha maarifa yake,
lakini wapumbavu hutangaza upumbavu wao.
24Kuwa na bidii kutampa mtu cheo,
lakini uvivu utamfanya mtumwa.
25Wasiwasi moyoni humkosesha mtu raha,
lakini neno jema humchangamsha.
26Mtu mwadilifu huuepa uovu,#12:26 Mtu mwadilifu … uovu: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
lakini njia ya waovu huwapotosha wenyewe.
27Mwindaji mvivu hatapata anachowinda,
lakini mwenye bidii atafanikiwa.#12:27 aya ya 27, makala ya Kiebrania si dhahiri.
28Uadilifu ni njia ya uhai,
lakini uovu huongoza katika mauti.#12:28 aya ya 28, makala ya Kiebrania si dhahiri.

Currently Selected:

Methali 12: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy