YouVersion Logo
Search Icon

Methali 1

1
Umuhimu wa methali
1 # Taz 1Fal 4:32 Hizi ni methali za Solomoni mfalme wa Israeli, mwana wa Daudi. 2Methali hizi zawapatia watu hekima na nidhamu; zawafanya waelewe maneno ya busara, 3zawafanya kuwa na nidhamu, utaratibu, uadilifu, haki na kutenda kwa usawa. 4Huwapatia wajinga werevu na vijana maarifa na hadhari. 5Mwenye hekima azisikie na kuongeza elimu yake, naye mwenye busara apate mwongozo. 6Mtu aelewe methali na mifano, maneno ya wenye hekima na vitendawili vyao.
7 # Taz Yobu 28:28; Zab 111:10; Meth 9:10 Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa maarifa,
lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.
Mawaidha kwa vijana
8Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,
wala usiyapuuze mafundisho ya mama yako;
9hayo yatakupamba kilemba kichwani pako,
kama mkufu shingoni mwako.
10Mwanangu, usikubali kushawishiwa na wenye dhambi.
11Wakisema: “Twende tukamvizie mtu na kumuua;
njoo tukawashambulie wasio na hatia!
12Tutawameza kama Kuzimu wakiwa hai,
watakuwa kama wale washukao Shimoni.
13Tutajitwalia mali zote za thamani,
nyumba zetu tutazijaza nyara.
14Njoo ushirikiane nasi,
vyote tutakavyopata tutagawana.”
15Wewe mwanangu usiandamane nao,
uzuie mguu wako usifuatane nao.
16Maana wao wako mbioni kutenda maovu,
haraka zao zote ni za kumwaga damu.
17Mtego utegwao huku ndege anaona,
mtego huo wategwa bure.
18Wao huvizia na kujiangamiza wao wenyewe,
hutega mtego wa kujinasa wao wenyewe.
19Ndivyo zilivyo njia za waishio kwa ukatili;
ukatili huyaangamiza maisha ya wakatili.
Hekima inaita
20 # Taz Meth 8:1-3 Hekima huita kwa sauti barabarani,
hupaza sauti yake sokoni;
21huita juu ya kuta,
hutangaza penye malango ya mji:#1:21 malango ya mji: Hapa ndipo mahali walipokutana watu kutatua matatizo na kesi zao.
22“Enyi wajinga! Mpaka lini mtapenda kuwa wajinga?
Mpaka lini wenye dharau watafurahia dharau zao,
na wapumbavu kuchukia maarifa?
23Sikilizeni maonyo yangu;
nitawamiminia mawazo yangu,
nitawajulisha maneno yangu.
24Kwa kuwa nimewaita mkakataa kusikiliza,
nimewapungia mkono mje mkakataa,
25mkapuuza mashauri yangu yote,
wala hamkuyajali maonyo yangu,
26nami pia nitayachekelea maafa yenu,
nitawadhihaki mnapokumbwa na hofu,
27hofu itakapowakumba kama tufani,
maafa yenu yatakapowavamia kama kimbunga,
wakati udhia na dhiki vitakapowapata.
28Hapo ndipo mtakaponiita lakini sitaitika;
mtanitafuta kwa bidii lakini hamtanipata.
29Kwa kuwa mliyachukia maarifa,
wala hamkuchagua kumcha Mwenyezi-Mungu;
30maadamu mlikataa shauri langu,
mkayapuuza maonyo yangu yote;
31basi, mtakula matunda ya mienendo yenu,
mtavimbiwa kwa hila zenu wenyewe.
32Maana wajinga hujiua kwa ukaidi wao,
wapumbavu hujiangamiza kwa kujiamini kwao.
33Lakini kila anisikilizaye atakaa salama,
atatulia bila kuogopa mabaya.”

Currently Selected:

Methali 1: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy