YouVersion Logo
Search Icon

Marko 11

11
Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mat 21:1-11; Luka 19:28-40; Yoh 12:12-19)
1Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake, 2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwanapunda amefungwa, ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete. 3Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnafanya hivyo?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara.’”
4Basi, wakaenda, wakamkuta mwanapunda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua, 5baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwanapunda?” 6Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao. 7Wakampelekea Yesu huyo mwanapunda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwanapunda na Yesu akaketi juu yake. 8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani. 9#Taz Zab 118:25-26 Watu wote waliotangulia na wale waliofuata, wakapaza sauti zao wakisema, “Sifa! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! 10Ubarikiwe ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Sifa kwa Mungu juu mbinguni!”
11Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
Yesu anaulaani mtini
(Mat 21:18-19)
12Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa. 13Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila tu majani matupu, kwa vile hayakuwa majira yake ya matunda. 14Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo.
Yesu anaingia hekaluni
(Mat 21:12-17; Luka 19:45-48; Yoh 2:13-22)
15Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu. 17Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi!”
18Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake. 19Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini.
Fundisho juu ya mtini ulionyauka
(Mat 21:20-22)
20Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi. 21Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!”
22Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu. 23Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo. 24Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa. 25Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu.” [ 26Lakini msipowasamehe wengine, hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe nyinyi makosa yenu.]
Suala kuhusu mamlaka ya Yesu
(Mat 21:23-27; Luka 20:1-8)
27Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea hekaluni, makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee walimwendea, 28wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?”
29Lakini Yesu akawaambia, “Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, nami pia nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. 30Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni.”
31Wakaanza kujadiliana, “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni’, atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’ 32Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.) 33Basi, wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”

Currently Selected:

Marko 11: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy