YouVersion Logo
Search Icon

Mika 7

7
Lalamiko la nabii
1Ole wangu!
Hali ilivyo ni kama baada ya mavuno;
hakuna tini za mwanzoni ninazotamani.
Ni kama wakati wa kuchuma zabibu
hakuna hata shada moja la zabibu la kula!
2Hakuna mcha Mungu aliyebaki nchini,
hakuna mtu yeyote mnyofu miongoni mwa watu.
Kila mmoja anavizia kumwaga damu;
kila mmoja anamwinda mwenzake amnase.
3Wote ni mabingwa wa kutenda maovu;
viongozi na mahakimu hutaka rushwa.
Wakubwa huonesha wazi nia zao mbaya,
na kufanya hila kuzitekeleza.
4Mwema zaidi kati yao hutaabisha kama mbigili,
aliye mnyofu zaidi ni kama ua wa miiba.
Siku iliyongojewa ya adhabu yao imefika.
Na sasa mahangaiko yamewakumba.
5Usimwamini mwenzako,
wala usimtumainie rafiki yako.
Chunga unachosema kwa mdomo wako,
hata na mke wako wewe mwenyewe.
6Maana, mtoto wa kiume anamdharau baba yake;
mtoto wa kike anashindana na mama yake,
mke wa mwana anapingana na mama mkwe wake.
Maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.
7Lakini mimi namtumainia Mwenyezi-Mungu,
namtazamia Mungu mwenye kuniokoa;
Mungu wangu atanisikiliza.
Tumaini na sala ya watu
8Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu!#7:8 hapa na aya zifuatazo yaani 9-10 nabii anaongea kwa niaba ya watu.
Nikianguka, nitainuka tena;
Nikiwa gizani, Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu.
9Kwa vile nimemkosea Mwenyezi-Mungu,
sina budi kuvumilia ghadhabu yake,
mpaka atakapotetea kisa changu
na kunijalia haki yangu.
Atanileta nje kwenye mwanga,
nami nitaona akithibitisha haki.
10Hapo adui yangu ataona hayo
naye atajaa aibu;
maana aliniambia: “Wapi basi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako?”
Mimi mwenyewe nitamwona adui akianguka;
atakanyagwakanyagwa chini kama tope la njiani.
11Siku yaja ambapo kuta za mji wenu zitajengwa upya.
Siku hiyo mipaka ya nchi yenu itapanuliwa.
12Siku hiyo ndugu zenu watawarudia,
kutoka Ashuru na vijiji vya Misri,
kutoka nchi ya Misri na eneo la Eufrate;
kutoka sehemu za maji na sehemu za milima.
13Lakini nchi yote nyingine itakuwa jangwa,
kwa sababu ya uovu wa wakazi wake.
Maombi
14Ee Mungu, uwachunge watu wako kwa fimbo yako,
uwachunge hao walio kundi lako mwenyewe
ambao wanaishi peke yao katika msitu
wamezungukwa na ardhi yenye rutuba.
Uwachunge kama ulivyofanya pale awali
katika malisho ya Bashani na Gileadi.
15Kama wakati ulipotutoa nchini Misri,
utuoneshe#7:15 Utuoneshe: Makala ya Kiebrania: Nitawaonyesheni. Katika aya 15 mpaka 20 nabii anaongea tena kwa niaba ya watu (taz pia aya 8-10). tena maajabu yako.
16Nao watu wa mataifa watakapoona hayo,
watajaa fedheha hata kama wana nguvu.
Watashikwa na bumbuazi na kukosa cha kusema
na kuwa kama viziwi.
17Watatambaa mavumbini kama nyoka;
naam, kama viumbe watambaao.
Watatoka katika ngome zao
huku wanatetemeka na kujaa hofu.
Watakugeukia wewe Mungu wetu kwa hofu,
wataogopa kwa sababu yako.
18Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?
Wewe wasamehe dhambi za watu wako waliobaki,
wala huyaangalii makosa yao.
Hasira yako haidumu milele,
ila wapendelea zaidi kutuonesha fadhili zako.
19Utatuhurumia tena, ee Mwenyezi-Mungu;
utafutilia mbali dhambi zetu,
utazitupa zote katika vilindi vya bahari.
20Utaonesha uaminifu wako na rehema zako
kwa wazawa wa Abrahamu na wa Yakobo,
kama ulivyowaahidi wazee wetu tangu zamani.

Currently Selected:

Mika 7: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy