YouVersion Logo
Search Icon

Mathayo 15

15
Mapokeo ya mababu
(Marko 7:1-13)
1Kisha Mafarisayo na waalimu wa sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza, 2“Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu? Hawanawi mikono ipasavyo kabla ya kula!” 3Yesu akawajibu, “Kwa nini nanyi hamjali sheria ya Mungu ila mnapendelea mapokeo yenu wenyewe? 4Mungu amesema: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima auawe.’ 5Lakini nyinyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema: ‘Kitu hiki nimemtolea Mungu,’ 6basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe. 7Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:
8‘Mungu asema: Watu hawa huniheshimu kwa maneno tu,
lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
9Kuniabudu kwao hakufai,
maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’”
Mambo yanayomtia mtu unajisi
(Marko 7:14-23)
10Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni, mkaelewe! 11Kitu kinachomtia mtu unajisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu unajisi.”
12Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?” 13Lakini yeye akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakupanda, utangolewa. 14Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni.” 15Petro akasema, “Tufafanulie huo mfano.” 16Yesu akasema, “Hata nyinyi hamwelewi? 17Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutolewa nje chooni? 18Lakini mambo yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. 19Maana moyoni hutoka mawazo ya uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa. 20Hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
Imani ya mama mmoja
(Marko 7:24-30)
21Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. 22Basi, mama mmoja Mkanaani wa nchi hiyo alimjia, akapaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.” 23Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele.” 24Yesu akajibu, “Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.” 25Hapo huyo mama akaja, akamsujudia, akasema, “Bwana, nisaidie.” 26Yesu akamjibu, “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” 27Huyo mama akajibu, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao.” 28Hapo Yesu akamjibu, “Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka.” Yule binti yake akapona wakati huohuo.
Yesu anawaponya watu wengi
29Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. 30Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. 31Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli.
Yesu anawapa chakula watu elfu nne
(Marko 8:1-10)
32Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.” 33Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?” 34Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba na visamaki vichache.” 35Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. 36Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. 37Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu saba. 38Hao waliokula walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. 39Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.

Currently Selected:

Mathayo 15: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy