YouVersion Logo
Search Icon

Yoeli 2

2
Nzige: Onyo juu ya siku ya Mwenyezi-Mungu
1Pigeni tarumbeta huko Siyoni;
pigeni baragumu juu ya mlima mtakatifu!
Tetemekeni enyi wakazi wa Yuda,
maana siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja,
naam, siku hiyo iko karibu!
2Hiyo ni siku ya giza na huzuni;
siku ya mawingu na giza nene.
Jeshi kubwa la nzige linakaribia
kama giza linalotanda milimani.
Namna hiyo haijapata kuweko kamwe
wala haitaonekana tena
katika vizazi vyote vijavyo.
3Kama vile moto uteketezavyo
jeshi hilo laharibu kila kitu mbele yake
na kuacha nyuma kila kitu kinateketezwa;
kabla hawajapita, nchi ni kama bustani ya Edeni,
lakini wakisha pita, ni jangwa tupu.
Hakuna kiwezacho kuwaepa!
4 # Taz Ufu 9:7-9 Wanaonekana kama farasi,
wanashambulia kama farasi wa vita,
5Wanaporukaruka kwenye vilele vya milima,
wanarindima kama magari ya farasi,
wanavuma kama mabua makavu motoni.
Wamejipanga kama jeshi kubwa
tayari kabisa kufanya vita.
6Wakaribiapo, watu hujaa hofu,
nyuso zao zinawaiva.
7Wanashambulia kama mashujaa wa vita;
kuta wanazipanda kama wanajeshi.
Wote wanakwenda mbele moja kwa moja,
bila hata mmoja wao kubadilisha njia.
8Hakuna amsukumaye mwenziwe;
kila mmoja anafuata mkondo wake.
Wanapita kati ya vizuizi vya silaha,
wala hakuna kiwezacho kuwazuia.
9Wanauvamia mji,
wanapiga mbio ukutani;
wanaziparamia nyumba na kuingia,
wanapenya madirishani kama wezi.
10 # Taz Ufu 8:12 Nchi inatetemeka mbele yao,
mbingu zinatikisika.
Jua na mwezi vyatiwa giza,
nazo nyota zinaacha kuangaza.
11 # Taz Ufu 6:17 Mwenyezi-Mungu anaamuru jeshi lake kwa sauti;
askari wake ni wengi mno,
wanaomtii hawahesabiki.
2Siku ya Mwenyezi-Mungu kweli ni kuu na ya kutisha sana!
Nani atakayeweza kuistahimili?
Wito wa toba
12“Lakini hata sasa,”
nasema mimi Mwenyezi-Mungu,
“Nirudieni kwa moyo wote,
kwa kufunga, kulia na kuomboleza.
13Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni
bali nirudieni kwa moyo wa toba.”
Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu;
yeye amejaa neema na huruma;
hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili;
daima yu tayari kuacha kuadhibu.
14Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia
na kuwapeni baraka ya mazao,
mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji.
15Pigeni tarumbeta huko Siyoni!
Toeni amri watu wafunge;
itisheni mkutano wa kidini.
16Wakusanyeni watu wote,
wawekeni watu wakfu.
Waleteni wazee,
wakusanyeni watoto,
hata watoto wanyonyao.
Bwana arusi na bibi arusi
na watoke vyumbani mwao.
17Kati ya madhabahu na lango la hekalu,
makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu,
walie na kuomba wakisema:
“Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu.
Usiyaache mataifa mengine yatudharau
na kutudhihaki yakisema,
‘Yuko wapi basi Mungu wao?’”
Mungu ataifanikisha nchi
18Ndipo Mwenyezi-Mungu akaipenda nchi yake
akawahurumia watu wake.
19Alisikiliza, akajibu sala zao; akasema,
“Sasa nitawapeni tena nafaka,
sitawafanya mdharauliwe tena na mataifa.
20Nitawaondoa hao adui watokao kaskazini,
nitawafukuza mpaka jangwani;
askari wa mbele nitawatupa katika Bahari ya Chumvi
na wale wa nyuma katika Bahari ya Mediteranea.
Watatoa uvundo na harufu mbaya,
hao ambao wamefanya maovu makubwa.
21“Usiogope, ewe nchi,
bali furahi na kushangilia,
maana Mwenyezi-Mungu ametenda makuu.
22Msiogope, enyi wanyama.
malisho ya nyikani yamekuwa mazuri,
miti inazaa matunda yake,
mizabibu na mitini zinazaa kwa wingi.
23“Furahini, enyi watu wa Siyoni,
shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
maana amewapeni mvua za masika,#2:23 mvua za masika: Au Mvua za masika kwa kuwa ni mwenye haki.
amewapeni mvua ya kutosha:
Mvua za masika na mvua za vuli kama hapo awali.
24Mahali pa kupuria patajaa nafaka,
mashinikizo yatafurika divai na mafuta.
25Nitawarudishia miaka ile iliyoliwa na nzige,
kila kitu kilicholiwa na tunutu, parare na matumatu,
hilo jeshi kubwa nililowaletea!
26Mtapata chakula kingi na kutosheka;
mtalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
aliyewatendea mambo ya ajabu.
Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena.
27Mtatambua kwamba mimi nimo miongoni mwenu,
enyi Waisraeli;
kwamba mimi Mwenyezi-Mungu,
ndimi Mungu wenu wala hakuna mwingine.
Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena.
Siku ya Mwenyezi-Mungu
28 # Taz Mate 2:17-21 # 2:28 katika Kiebrania sura ya 3 yaanza hapa. “Kisha hapo baadaye
nitaimimina roho yangu juu ya binadamu wote.
Watoto wenu wa kike na wa kiume watatabiri,
wazee wenu wataota ndoto,
na vijana wenu wataona maono.
29Hata juu ya watumishi wa kiume na wa kike,
nitaimimina roho yangu wakati huo.
30“Nitatoa ishara mbinguni na duniani;
kutakuwa na damu, moto na minara ya moshi.
31 # Taz Mat 24:29; Marko 13:24-25; Luka 21:25: Ufu 6:12-13 Jua litatiwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kufika siku ya Mwenyezi-Mungu,
siku iliyo kuu na ya kutisha.
32 # Taz Rom 10:13 Hapo watu wote watakaoomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu wataokolewa.
Maana katika mlima Siyoni na Yerusalemu,
watakuwako watu watakaosalimika,
kama nilivyosema mimi Mwenyezi-Mungu.

Currently Selected:

Yoeli 2: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy