YouVersion Logo
Search Icon

Yobu 33

33
1“Sasa, Yobu, sikiliza hoja yangu;
sikiliza maneno yangu yote.
2Tazama, nafumbua kinywa changu,
naam, ulimi wangu utasema.
3Nitasema kadiri ya unyofu wa moyo wangu;
ninayoyajua nitayasema kwa uaminifu.
4Roho ya Mungu iliniumba,
nayo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu yanipa uhai.
5Nijibu, kama unaweza.
Panga hoja zako vizuri mbele yangu,
ushike msimamo wako.
6Wewe na mimi ni sawa mbele ya Mungu;
mimi pia niliumbwa kwa sehemu ya udongo.
7Kwa hiyo huna sababu ya kuniogopa;
maneno yangu mazito hayatakulemea.
8Kweli umesema, nami nikasikia;
nimeyasikia yote uliyosema.
9Wewe umesema, u safi na wala huna kosa,
u safi kabisa na huna hatia;
10umesema kwamba Mungu anakutafutia kisa,
na kukuona kama adui yake.
11 # Taz Yobu 13:27 Anakufunga miguu minyororo,
na kuchunguza hatua zako zote.
12“Lakini Yobu, nakuambia hapo umekosea.
Mungu ni mkuu kuliko binadamu.
13Kwa nini unashindana naye,
ukisema hatajibu swali lako moja?
14Mungu anaposema hutumia njia moja,
au njia nyingine lakini mtu hatambui.
15 # Taz Yobu 4:13 Mungu huongea na watu katika ndoto na maono,
wakati usingizi mzito unapowavamia,
16wanaposinzia vitandani mwao.
Hapo huwafungulia watu masikio yao;
huwatia hofu kwa maonyo yake,
17wapate kuachana na matendo yao mabaya,
na kuvunjilia mbali kiburi chao.
18Hivyo humkinga mtu asiangamie shimoni,
maisha yake yasiangamie kwa upanga.
19“Mungu humrudi mtu kwa maumivu yamwekayo kitandani,
maumivu hushika viungo vyake bila kukoma;
20naye hupoteza hamu yote ya chakula,
hata chakula kizuri humtia kinyaa.
21Mwili wake hukonda hata asitambuliwe,
na mifupa yake iliyofichika ikatokeza nje.
22Yuko karibu sana kuingia kaburini,
na maisha yake karibu na wale waletao kifo.
23Lakini malaika akiwapo karibu naye,
mmoja kati ya maelfu ya watetezi wa Mungu,
ili kumwonesha lililo jema la kufanya,
24akamwonea huruma na kumwambia Mungu;
‘Mwokoe asiingie Shimoni,
ninayo fidia kwa ajili yake.’
25Hapo mwili wake utaweza kuwa tena kama kijana,
ataweza kurudia tena nguvu zake za ujana.
26Kisha atamwomba Mungu na kukubaliwa,
atakuja mbele yake kwa furaha,
na Mungu atamrudishia fahari yake.
27Atashangilia mbele ya watu na kusema:
‘Nilitenda dhambi na kupotosha haki,
nami sikuadhibiwa kutokana na hayo.
28Mungu aliniokoa nisiangamie Shimoni;
nimebaki hai na ninaona mwanga.’
29“Tazama Mungu humfanyia binadamu haya yote,
tena mara mbili, mara tatu.
30Humwokoa binadamu asiangamie Shimoni,
aweze kuona mwanga wa maisha.
31Sikia Yobu, nisikilize kwa makini;
kaa kimya, nami nitasema.
32Kama una la kusema, nijibu;
sema, maana nataka kukuona huna hatia.
33La sivyo, nyamaza unisikilize,
kaa kimya nami nikufunze hekima.”

Currently Selected:

Yobu 33: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy