YouVersion Logo
Search Icon

Yeremia 30

30
Ahadi za Mungu kwa watu wote
1Neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu: 2“Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Yaandike katika kitabu maneno yote niliyokuambia. 3Maana siku zaja ambapo nitawarudishia fanaka zao watu wangu wa Israeli na Yuda na kuwarudisha katika nchi niliyowapa wazee wao, nao wataimiliki. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
4Haya ndiyo mambo aliyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu watu wa Israeli na Yuda:
5“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Kumesikika kilio cha hofu
sauti ya kutisha wala si ya amani.
6Jiulizeni sasa na kufahamu:
Je, mwanamume aweza kujifungua mtoto?
Mbona basi, namwona kila mwanamume
amejishika kiunoni kama mwanamke mwenye utungu
na nyuso zao zimegeuka rangi?
7Kweli, siku hiyo ni kubwa,
hakuna nyingine kama hiyo;
ni siku ya huzuni kwa watu wa Yakobo;
hata hivyo, wataokolewa humo.
8“Siku hiyo itakapofika, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nitaivunja nira iliyo shingoni mwao na kukata minyororo yao. 9Nao hawatakuwa tena watumwa wa wageni, bali watanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, na mfalme wa ukoo wa Daudi ambaye nitawateulia.
10“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Usiogope ee Yakobo mtumishi wangu,
wala usifadhaike, ee Israeli;
maana nitakuokoa huko mbali uliko,
na wazawa wako kutoka uhamishoni.
Utarudi na kuishi kwa amani,
wala hakuna mtu atakayekuogopesha.
11Maana mimi niko pamoja nawe, kukuokoa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Nitayaangamiza kabisa mataifa yote,
ambayo nilikutawanya kati yao;
lakini wewe sitakuangamiza kabisa.
Nitakuadhibu kadiri unavyostahili
wala sitakuacha uende bila kukuadhibu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
12“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Majeraha yako hayaponyeki,
vidonda vyako havitibiki.
13Hakuna atakayeshughulikia kisa chako,
jeraha lako halina dawa,
wewe hutaponyeshwa.
14Wapenzi wako wote wamekusahau;
hawajali chochote juu yako,
nimekupiga pigo la adui;
umeadhibiwa bila huruma,
kwa kuwa kosa lako ni kubwa,
dhambi zako ni nyingi mno.
15Mbona unalia juu ya jeraha lako?
Maumivu yako hayaponyeki.
Nimekutendea hayo yote,
kwa sababu kosa lako ni kubwa,
dhambi zako ni nyingi mno.
16Lakini wote wanaokuangamiza, wataangamizwa,
na maadui zako wote watachukuliwa uhamishoni;
wanaokuteka nyara, watatekwa nyara,
wanaokuwinda nitawawinda.
17“Nitakurudishia afya yako,
na madonda yako nitayaponya,
japo wamekuita ‘Aliyetupwa’,
‘Mji Siyoni usio na wa kuutunza!’”
18Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nitazirudisha tena fanaka za maskani ya Yakobo,
na kuyaonea huruma makao yake;
mji utajengwa upya juu ya magofu yake,
na ikulu ya mfalme itasimama pale ilipokuwa.
19Humo zitatoka nyimbo za shukrani
na sauti za wale wanaosherehekea.
Nitawaongeza na wala hawatakuwa wachache;
nitawafanya waheshimiwe wala hawatadharauliwa.
20Watoto wao watakuwa kama walivyokuwa zamani,
jumuiya yao itaimarika mbele yangu,
nami nitawaadhibu wote wanaowakandamiza.
21Kiongozi wao atakuwa mmoja wao,
mtawala wao atatokea miongoni mwao.
Nitamleta karibu naye atanikaribia;
maana, nani anayethubutu kunikaribia kwa nguvu zake?
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
22Nanyi mtakuwa watu wangu,
nami nitakuwa Mungu wenu.”
23Tazama, dhoruba kali kutoka kwa Mwenyezi-Mungu!
Ghadhabu imezuka,
kimbunga cha tufani
kitamlipukia mtu mwovu kichwani.
24Hasira ya Mwenyezi-Mungu haitarudi nyuma,
mpaka atakapotekeleza na kukamilisha
matakwa ya moyo wake.
Siku zijazo mtayaelewa vema mambo hayo.

Currently Selected:

Yeremia 30: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy