YouVersion Logo
Search Icon

Waamuzi UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu hiki kinajulikana kwa jina la Waamuzi, lakini mkazo wa masimulizi yaliyomo ni juu ya mambo ambayo hao viongozi wa watu waliyatekeleza. Ama kwa kweli hao hawakuwa “Waamuzi” kwa maana yake kamili katika lugha yetu bali walikuwa viongozi wa kivita nyakati za misukosuko na pia nyakati za amani. Hao viongozi wa makabila walizuka huko Kanaani kuanzia wakati baada ya Waisraeli kuimiliki nchi hiyo mpaka wakati walipojipatia mfalme wa kwanza (yaani labda kati ya mwaka 1200 na 1000 K.K.).
Kitabu hiki basi, kina kumbukumbu ya mambo waliyotenda viongozi hao katika hali mbalimbali nchini humo kabla ya kuanzishwa kwa utawala wa kifalme. Kabla ya hapo kila mtu alifanya alichotaka (tazama 17:6; 18:1; 21:25).
Katika kitabu hiki tunaambiwa tena na tena kwamba kufanikiwa au kuangamia kwa Waisraeli kulitegemea uaminifu wao kwa Mungu. Uasi kwa Mungu husababisha maangamizi, bali uaminifu na kumtegemea Mungu huleta fanaka. Misukosuko iliyowakumba Waisraeli inaelezwa kwa mpango maalumu wa ufasaha: Waisraeli walikosa uaminifu kwa Mungu, naye Mungu akawaacha waadhibiwe na maadui zao – walimlilia Mungu, naye Mungu akawapelekea viongozi wa kuwaokoa (tazama kwa mfano 2:11-16; 3:7-11; 4:1-3; 4:23-24; 6:1-10; 10:6-16).
Kitabu chenyewe kina sehemu tatu:
Sura 1:1-2:5: Hapa tunapewa picha nyingine ya hali nchini Kanaani tofauti na picha tuliyopewa katika kitabu cha Yoshua. Tunaambiwa pia kwamba wengi wa wakazi wa Kanaani baada ya Waisraeli kuiteka hiyo nchi hawakuangamizwa; waliachwa kwa vile Mungu alitaka kuwatumia kuwajaribu watu wake kama kwa kweli wangebaki waaminifu kwake (tazama 2:3, 23; na 3:4).
Sura 2:6–16:31: Sehemu hii ni kitovu cha kitabu hiki. Hapa tuna masimulizi juu ya waamuzi maarufu: Othnieli, Ehudi, Shamgari, Debora, Baraki, Gideoni, Yeftha na Samsoni, na pia juu ya waamuzi wadogo: Abimeleki, Tola, Yairi, Ibshani, Eloni na Abdoni.
Sura 17–21: Katika sehemu hii tunapewa picha ya jinsi mambo yalivyokuwa mabaya nyakati hizo, wakati ambapo Waisraeli hawakuwa na mfalme bado. Bila shaka mwandishi alitaka kubainisha tofauti ya nyakati hizo na nyakati za fanaka na ustawi za mfalme Daudi na Solomoni.

Currently Selected:

Waamuzi UTANGULIZI: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy