YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 3

3
Msukosuko Yerusalemu
1Sasa, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi
ataondoa kutoka Yerusalemu na Yuda kila tegemeo:
Tegemeo lote la chakula,
na tegemeo lote la kinywaji.
2Ataondoa mashujaa na askari,
waamuzi na manabii,
waaguzi na wazee,
3majemadari wa vikosi vya watu hamsini,
na watu wenye vyeo,
washauri, wachawi stadi na walozi hodari.
4Mungu ataweka watoto wawatawale;
naam, watoto wachanga watawatawala.
5Watu watadhulumiana,
kila mtu na jirani yake;
vijana watawadharau wazee wao,
na watu duni watapuuza wakuu wao.
6Wakati huo ndugu atamwambia ndugu yake
wakiwa bado nyumbani kwa baba yao:
“Wewe unalo koti;
utakuwa kiongozi wetu.
Chukua hatamu juu ya uharibifu huu!”
7Lakini siku hiyo atasema,
“Mimi siwezi kuwa mwuguzi,
nyumbani mwangu hamna chakula wala mavazi.
Msinifanye mimi kuwa kiongozi wenu.”
8Watu wa Yerusalemu wamejikwaa,
watu wa Yuda wameanguka,
kwa kuwa wanampinga Mwenyezi-Mungu
kwa maneno na matendo,
wakipuuza utukufu wake miongoni mwao.
9Ubaguzi wao unashuhudia dhidi yao;
wanatangaza dhambi yao kama ya Sodoma,
wala hawaifichi.
Ole wao watu hao,
kwani wamejiletea maangamizi wenyewe.
10Waambieni waadilifu jinsi walivyo na bahati:
Kwani watakula matunda ya matendo yao.
11Lakini ole wao watu waovu!
Mambo yatawaendea vibaya,
kwani waliyotenda yatawapata wao wenyewe.
12Watu wangu watadhulumiwa na watoto;
wanawake ndio watakaowatawala.
Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,
wanavuruga njia mnayopaswa kufuata.
Mwenyezi-Mungu awahukumu watu wake
13Mwenyezi-Mungu yu tayari kuanza mashtaka,
anasimama kuwahukumu watu wake.
14Mwenyezi-Mungu anawashtaki
wazee na wakuu wa watu wake:
“Nyinyi ndio mlioliharibu shamba la mizabibu;
mali walizowanyanganywa maskini zimo nyumbani kwenu.
15Mnamaanisha nini kuwakandamiza watu wangu,
kuwatendea ukatili watu maskini?
Nauliza mimi Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.”
Onyo kwa wanawake wa Yerusalemu
16Mwenyezi-Mungu asema:
“Wanawake wa Siyoni wana kiburi;
wanatembea wameinua shingo juu,
wakipepesa macho yao kwa tamaa.
Hatua zao ni za maringo,
na miguuni njuga zinalia.
17Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitawaadhibu;
nitawanyoa nywele hao wanawake wa Siyoni,
na kuwavua nguo za kufunika uchi wao.”
18Siku yaja ambapo Mwenyezi-Mungu atawanyanganya wanawake wa Yerusalemu vitu vyote wanavyoringia: Njuga, kaya, mikufu, 19vipuli, vikuku, shungi, 20vitambaa vya kichwani, bangili, vibwebwe, vibweta vya marashi, hirizi, 21pete, hazama, 22mavazi ya sikukuu, mitandio, majoho, mikoba, 23mavazi yaoneshayo, mavazi ya kitani, vilemba na shela.
24Badala ya kunukia marashi watatoa uvundo;
badala ya mishipi mizuri watatumia kamba;
badala ya nywele nzuri watakuwa na upara;
badala ya mavazi mazuri watavaa matambara;
uzuri wao wote utageuka kuwa aibu.
25Wanaume wenu wataangamia kwa upanga,
watu wenu wenye nguvu watakufa vitani.
26Malango ya mji yatalia na kuomboleza;
nao mji utakuwa kama mwanamke aliyepokonywa kila kitu, ameketi mavumbini.

Currently Selected:

Isaya 3: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy