YouVersion Logo
Search Icon

Kutoka 23

23
Haki na usawa
1“Usitoe habari za uongo. Usishirikiane na mtu mwovu ili kuwa shahidi mbaya. 2Usifuate genge la watu kutenda uovu, wala usijumuike na genge la watu kutoa ushahidi mahakamani ili kupotosha haki. 3#Taz Lawi 19:15 Usiwe na upendeleo katika kesi ya maskini.
4“Ukimkuta ng'ombe au punda wa adui yako amepotea, utamrudishia mwenyewe. 5Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako.
6“Usiipotoshe haki anayostahili maskini katika kesi yake. 7Jitenge mbali na mashtaka ya uongo wala usiwaue wasio na hatia na waadilifu, maana mimi sitamsamehe mtu mwovu. 8Usipokee rushwa, maana rushwa huwapofusha wakuu na kupotosha mambo ya wenye haki.
9“Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri.
Mwaka wa saba
10“Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake. 11Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.
12“Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe. 13Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako.
Sikukuu tatu kubwa
(Kut 34:18-26; Kumb 16:1-17)
14“Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu. 15#Taz Kut 12:14-20; Lawi 23:6-8; Hes 28:17-25 Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu. 16#Taz Lawi 23:15-21, 39-43; Hes 28:26-31 Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno#23:16 sikukuu ya kukusanya mavuno: Au sikukuu ya vibanda. mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu. 17Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.
18“Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi.
19 # Taz Kut 34:26; Kumb 14:21; 26:2 “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.
“Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.#23:19 desturi hiyo ilifanyika katika mila za kidini za Wakanaani.
Ahadi na maagizo
20“Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia. 21Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu. 22Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu. 23Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nikawaangamiza hao wote, 24msiiname mbele ya miungu yao kuiabudu, wala kuitumikia, wala msiige mambo yao. Bali mtawaangamiza kabisa na kuzivunjavunja nguzo zao. 25Mtanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawabariki kwa chakula na maji na kuyaondoa magonjwa kati yenu. 26Hakutakuwa na mwanamke yeyote atakayepoteza mimba wala kuwa tasa katika nchi yenu. Nami nitawajalia maisha marefu.
27“Nitapeleka kitisho mbele yenu na kuwavuruga watu wote mtakaowakabili, na adui zenu nitawafanya wageuke na kuwakimbia. 28Nitapeleka manyigu mbele yenu ambao watawafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti. 29Sitawaondoa watu hao katika mwaka mmoja, nchi isije ikabaki tupu na wanyama wa porini wakaongezeka mno na kuwazidi nguvu. 30Lakini nitawaondoa kidogokidogo mpaka hapo mtakapoongezeka na kuimiliki nchi hiyo. 31Mipaka ya nchi yenu itakuwa kutoka bahari ya Shamu hadi bahari ya Mediteranea, na kutoka jangwani mpaka mto Eufrate, maana nitawatia wakazi wa nchi hiyo mikononi mwenu, nanyi mtawafukuza wawaondoke. 32Msifanye agano lolote nao, wala na miungu yao. 33Msiwaruhusu waishi nchini mwenu wasije wakawafanya mtende dhambi dhidi yangu; maana kama mkiitumikia miungu yao, hakika hiyo itakuwa mtego wa kuwanasa.”

Currently Selected:

Kutoka 23: BHN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy