YouVersion Logo
Search Icon

1 Wathesalonike UTANGULIZI

UTANGULIZI
Wakati wa Paulo, mji wa Thesalonike ulikuwa mji mkuu wa mkoa wa Makedonia, sasa ni sehemu ya kaskazini-mashariki ya nchi ya Ugiriki. Thesalonike ulikuwa mji maarufu na bandari katika pwani ya Bahari ya Ageo.
Paulo na wenzake, wahubiri wa Habari Njema ya Kristo, walikuwa wa kwanza kabisa kuwaletea watu wa Europa Injili. Baada ya kutua katika Bandari ya Troade na Apolonia, wakati wa ziara yake ya pili ya kuhubiri, alifika Thesalonike (Mate 17:1; 1Thes 2:1-2), akaanzisha jumuiya ya waumini wa Kristo. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinatupa habari kwamba Paulo alijadiliana na Wayahudi huko Thesaloinike kwa Sabato tatu mfululizo (Mate 17:2). Inaonekana kwamba Paulo alikaa huko yapata miezi mitatu kulingana na matukio yanayotajwa katika Mate 17:4-9; rejea pia Fil 4:16 kuhusu msaada waumini wa Filipo waliompelekea Paulo huko Thesalonike (walimpelekea msaada mara mbili). Baadhi ya Wayahudi wa huko, kundi kubwa la Wagiriki waliomcha Mungu na wanawake wengi, waliamini (Mate 17:4). Hiyo ilisababisha upinzani mkali kutoka kwa Wayahudi wengine kwani watu mashuhuri, wanaume kwa wanawake, ambao hapo awali walikuwa wameunga mkono dini ya Kiyahudi, waliongoka wakawa Wakristo (Mate 17:1-9). Basi, ilimlazimu Paulo kuondoka haraka.
Kutoka Thesalonike, Paulo alikwenda Berea (Mate 17:10). Kisha Athene (Mate 17:15) na mwishowe Korintho (Mate 18:1) ambako, yapata mwaka wa 50 B.K. aliandika Barua hii ya Kwanza kwa Wathesalonike (1Thes 3:6; rejea Mate 18:5). Paulo alikuwa na nia ya kurudi tena huko Thesalonike lakini hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo alimtuma Timotheo kutoka Athene na kumwagiza awatie moyo waumini wa huko Thesalonike na atakapokutana nao amfahamishe juu ya maendeleo ya Kanisa la huko. Timotheo alifanya safari hiyo na kurudi Korintho. Habari alizompatia Paulo kuhusu Thesalonike zilikuwa nzuri kwa jumla ingawa waumini wa huko hawakuwa wamekomaa katika imani. Paulo alifurahi kwa habari hizo na akaandika Barua hii.
Hii ni Barua ya kale miongoni mwa Barua zote za Paulo; nao wataalamu wa Maandiko Matakatifu wanahisi ni maandishi ya kwanza kabisa tuliyokabidhiwa katika A.J.
Barua hii ya kwanza ina shukrani za Paulo kwa habari nzuri alizopata juu ya imani na upendo wa jumuiya ya Thesalonike. Paulo anawakumbusha waumini ile ziara yake huko. Kisha anawashauri kuhusu masuala yao, aghalabu juu ya kuja kwake Kristo. Paulo anasisitiza kila mtu aendelee na kazi zake kwa utulivu lakini katika matumaini. Anawapa pia mawaidha yake kuhusu ufufuo wa wafu.

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy