Marko 7:31-37
Marko 7:31-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli. Basi, wakamletea bubu kiziwi, wakamwomba amwekee mikono. Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi. Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake “Funguka.” Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa. Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo. Watu walishangaa sana, wakasema, “Amefanya yote vyema: Amewajalia viziwi kusikia, na mabubu kusema!”
Marko 7:31-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka ziwa la Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.
Marko 7:31-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.
Marko 7:31-37 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Yesu akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli. Huko, watu wakamletea Yesu mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu na amponye. Baadaye Yesu akampeleka yule kiziwi kando mbali na watu, Yesu akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. Ndipo Yesu akatazama mbinguni, akavuta hewa ndani kwa nguvu akamwambia, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”) Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa. Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowazuia, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii. Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”