Marko 7:24-30
Marko 7:24-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha. Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake. Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu. Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.” Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!” Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.
Marko 7:24-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake ana pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Mgiriki, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, nenda zako, pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.
Marko 7:24-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.
Marko 7:24-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha. Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake. Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu. Yesu akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.” Ndipo Yesu akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.” Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.