Yona 4:4-8
Yona 4:4-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Naye Mwenyezi-Mungu akamjibu Yona: “Unadhani wafanya vema kukasirika?” Ndipo Yona akatoka nje ya mji, akajikalia upande wa mashariki wa mji huo. Hapo, akajijengea kibanda, akaketi kivulini mwake huku anangojea apate kuona litakaloupata mji wa Ninewi. Mungu, Mwenyezi-Mungu akaamuru mmea uote na kukua. Akauotesha ili kumpatia Yona kivuli cha kumpunguzia taabu aliyokuwa nayo. Yona akaufurahia sana mmea huo. Lakini siku ya pili, kulipopambazuka, Mungu akaamuru mdudu auharibu mmea huo, ukanyauka. Jua lilipochomoza, Mungu akaleta upepo wa hari kutoka mashariki, jua likamchoma sana Yona kichwani, karibu azirai. Yona akasema, “Afadhali kufa kuliko kuishi!”
Yona 4:4-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye BWANA akasema, Je! Unatenda vema kukasirika? Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajitengenezea kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hadi aone mji ule utakuwaje. Na BWANA Mungu aliutayarisha mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango. Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akatayarisha buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakatika. Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akatayarisha upepo wa mashariki, wenye joto jingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
Yona 4:4-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye BWANA akasema, Je! Unatenda vema kukasirika? Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje. Na BWANA Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango. Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akaweka tayari buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakatika. Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akaweka tayari upepo wa mashariki, wenye hari nyingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
Yona 4:4-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini BWANA akamjibu, “Je unayo haki yoyote kukasirika?” Yona akatoka nje akaketi mahali upande wa mashariki wa mji. Hapo akajitengenezea kibanda, akaketi kwenye kivuli chake na kungojea ni nini kitakachotokea katika mji. Ndipo BWANA, Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu. Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka. Wakati jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona mpaka akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”