Yohane 5:5-9
Yohane 5:5-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo na kujua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, “Je, wataka kupona?” Naye akajibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia.” Yesu akamwambia, “Inuka, chukua mkeka wako utembee.” Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.
Yohane 5:5-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa mgonjwa muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa katika hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia katika bwawa, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.
Yohane 5:5-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.
Yohane 5:5-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwa hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?” Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.” Yesu akamwambia, “Inuka! Chukua mkeka wako na uende.” Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea. Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.