Yohane 5:41-47
Yohane 5:41-47 Biblia Habari Njema (BHN)
“Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu. Lakini nawajua nyinyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea. Mwawezaje kuamini, hali nyinyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu nyinyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu? Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye nyinyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki. Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia, maana Mose aliandika juu yangu. Lakini hamyaamini yale aliyoandika; mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?”
Yohane 5:41-47 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Lakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. Mnawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini maneno yangu vipi?
Yohane 5:41-47 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?
Yohane 5:41-47 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Mimi sitafuti kutukuzwa na wanadamu. Lakini ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei, lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea. Ninyi mwawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamna bidii kupata utukufu utokao kwa Mungu? “Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba, mshtaki wenu ni Mose, ambaye mmemwekea tumaini lenu. Kama mngelimwamini Mose, mngeliniamini na mimi kwa maana aliandika habari zangu. Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Mose, mtaaminije ninayoyasema?”