Waebrania 6:7-12
Waebrania 6:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima imebarikiwa na Mungu. Ardhi ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto. Ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tuna uhakika wa kupewa mambo mema zaidi: Yaani wokovu. Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mliyoonesha kwa ajili yake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake. Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aoneshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia. Hivyo msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu, wakapokea yale aliyoahidi Mungu.
Waebrania 6:7-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao inalimwa, hupokea baraka zitokazo kwa Mungu; bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa. Lakini, wapenzi, ijapokuwa twanena hayo, kuhusu habari zenu tumeamini mambo yaliyo mazuri zaidi, na yaliyo na wokovu. Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe kama hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu.
Waebrania 6:7-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu; bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa. Lakini, wapenzi, ijapokuwa twanena hayo, katika habari zenu tumesadiki mambo yaliyo mazuri zaidi, na yaliyo na wokovu. Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu.
Waebrania 6:7-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ardhi ile ipokeayo mvua inyeshayo juu yake mara kwa mara hutoa mazao yanayowanufaisha wale ambao kwa ajili yao yalimwa, nayo nchi hiyo hupokea baraka kutoka kwa Mungu. Lakini ardhi ikizaa miiba na mibaruti, haina thamani na iko hatarini ya kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto. Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mema zaidi, mambo yale yahusuyo wokovu. Mungu si mdhalimu: yeye hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na hata sasa mnaendelea kuwahudumia. Nasi twataka kila mmoja wenu aonyeshe bidii iyo hiyo ili mpate kujua uhakika kamili wa lile tumaini mpaka mwisho, ili msije mkawa wavivu, bali mpate kuwaiga wale ambao kwa imani na saburi hurithi zile ahadi.