Matendo 19:14-17
Matendo 19:14-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Watoto saba wa Skewa, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha. Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.
Matendo 19:14-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Walikuwapo wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile wakiwa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wagiriki waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa.
Matendo 19:14-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa. Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa.
Matendo 19:14-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha. Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana.