2 Timotheo 1:10-14
2 Timotheo 1:10-14 Biblia Habari Njema (BHN)
lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uhai usio na kifo. Mimi nimechaguliwa niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema, nami nateseka kwa mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye atakilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka siku ile. Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu. Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu.
2 Timotheo 1:10-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutoharibika, kwa ile Injili; kwa ajili ya Injili hiyo niliwekwa niwe mhubiri, mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, lakini sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile. Shika mfano wa mafundisho ya kweli uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.
2 Timotheo 1:10-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.
2 Timotheo 1:10-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili. Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile. Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima yale uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.