1 Wathesalonike 4:9-12
1 Wathesalonike 4:9-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Nyinyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana. Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu, tunawaombeni mfanye hata zaidi. Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.
1 Wathesalonike 4:9-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuhusu upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Kwa maana mnafanya neno hili kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini tunawasihi, ndugu, mzidi sana. Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza; ili mwende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu chochote.
1 Wathesalonike 4:9-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Kwa maana mnafanya neno hili kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini twawasihi, ndugu, mzidi sana. Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza; ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu cho chote.
1 Wathesalonike 4:9-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda. Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.