Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isa 40

40
Watu wa Mungu Wafarijiwa
1Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu. 2Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa BWANA adhabu maradufu kwa dhambi zake zote.
3 # Mal 3:1; Lk 1:76; Mt 3:3; Mk 1:3; Yn 1:23 Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye,
Itengenezeni nyikani njia ya BWANA;
Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.
4Kila bonde litainuliwa,
Na kila mlima na kilima kitashushwa;
Palipopotoka patakuwa pamenyoka,
Na palipoparuza patasawazishwa;
5 # Kut 16:7; Zab 72:19; Eze 36:23; Lk 2:10 Na utukufu wa BWANA utafunuliwa,
Na wote wenye mwili watauona pamoja;
Kwa kuwa kinywa cha BWANA kimenena haya.
6 # Yak 1:10-11; 1 Pet 1:24-25 Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia!
Nikasema,
Nilie nini? Wote wenye mwili ni majani,
Na wema wake wote ni kama ua la kondeni;
7Majani yakauka, ua lanyauka;
Kwa sababu pumzi ya BWANA yapita juu yake.
Yakini watu hawa ni majani.
8Majani yakauka, ua lanyauka;
Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.
9Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema,
Panda juu ya mlima mrefu;
Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema,
Paza sauti kwa nguvu;
Paza sauti yako, usiogope;
Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu.
10 # Isa 62:11; Ufu 22:12 Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa,
Na mkono wake ndio utakaomtawalia;
Tazameni, thawabu yake i pamoja naye,
Na ijara yake i mbele zake.
11 # Eze 34:15,23; Isa 49:10; Ebr 13:20; 1 Pet 2:25; Ufu 7:17; Yn 10:11 Atalilisha kundi lake kama mchungaji,
Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake;
Na kuwachukua kifuani mwake,
Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.
12Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiri mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani? 13#Rum 11:34; 1 Kor 2:16Ni nani aliyemwongoza roho ya BWANA, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake? 14Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonyesha njia ya fahamu? 15Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana. 16Lebanoni nayo hautoshi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara. 17Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni ya si kitu, na ubatili. 18#Mdo 17:29Basi, mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani? 19Sanamu fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha. 20#Yer 10:4Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi mstadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika. 21#Zab 19:1; Mdo 14:17; Rum 1:19Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia? 22#Mwa 1:1,6; Ayu 9:8; Zab 104:2; Yer 10:12Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa; 23#Ayu 12:21ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia. 24Naam, hawakupandwa; hawakutiwa katika ardhi kama mbegu; naam, shina lao halikutia mizizi katika ardhi; tena awapuzia tu, wakanyauka, upepo wa kisulisuli wawaondoa kama mabua makavu. 25#Kum 4:15; Isa 40:18; Mdo 17:24-29Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu. 26#Zab 147:4Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.
27Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, BWANA asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie? 28#Zab 147:5; Rum 11:33Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. 29Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. 30Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; 31#Ayu 17:9; Zab 25:3; Isa 8:17; Omb 3:25; 2 Kor 4:8-10,16bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Iliyochaguliwa sasa

Isa 40: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha